January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kairuki atumbua jipu Chuo cha Utumishi

Spread the love

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki amewasimamisha kazi watumishi watendaji waandamizi watatu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) akiwemo Mtendaji Mkuu, kwa kuwahusisha na ubadhirifu wa fedha za umma. Anaandika Happyness Lidwino.

Waziri Kairuki amemsimamisha Mtendaji Mkuu wa TPSC, Said Nasoro kwa kushindwa kusimamia ipasavyo wasaidizi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, waziri amesema mbali na Nasoro, ambaye alihudhuria mkutano na waandishi wa habari, amewasimamisha kazi Silivanusi Ngata, Mkuu wa Chuo hicho Tawi la Tabora na Joseph Mbwilo, Mkuu wa chuo Tawi la Dar es Salaam.

Waziri Kairuki amesema watendaji hao wamehusika na ubadhirifu wa fedha za umma ambapo alipokea malalamiko kwa viongozi wenzao na akajiridhisha kuwa “hawana sifa” ya kuwa watumishi wa umma.

Akimzungumzia Mbwilo, Kairuki amesema mnamo mwaka 2013 wakati akiwa Tabora alitumia vibaya kiasi cha Sh. Bilioni moja zilizotokana na ada za wanafunzi. Hakuchukuliwa hatua na Mtendaji Mkuu wa TPSC, badala yake alimpandisha cheo kuwa Kaimu Mkuu wa Utawala na Fedha, Tawi la Dar es Salaam.

Kuhusu Ngata, waziri amesema anatuhumiwa kuwa kati ya mwaka 2011 na 2013 alipokuwa Tawi la Mtwara alifanya ubadhirifu wa fedha kwa kuongeza ghorofa mbili za jengo la chuo lakini naye badala ya kuchukuliwa hatua, alihamishiwa Tawi la Tabora.

“Pamoja na makosa hayo yote kutendeka, Nasoro aliyajua lakini kutokana na utendaji wake kutokuwa na ufanisi aliwaachia na kuwaongeza vyeo. Kwa hivyo ubadhirifu huu uliongozwa na yeye,” amesema.

Waziri Kairuki amesema amechukua hatua kwa mamlaka aliyonayo kisheria kupitia sheria za kazi kwa watumishi wa serikali Na. 245 na kusisitiza kuwa “Tutaendelea na mchakato huu hadi wote watakate.”

Katika hali iliyoonesha mshangao, Waziri Kairuki amechukua hatua dhidi ya Nasoro wakati mwenyewe hakuwa na habari ya kilichokuwa kinakwenda kutekelezwa katika mkutano huo.

Waandishi walishangaa walipouliza watendaji waliosimamishwa wako wapi, hasa baada ya Waziri Kairuki kukataa kuulizwa maswali, ndipo mfanyakazi wa wizarani alipowaonesha waandishi mtendaji Nasoro ambaye alisema “siwezi kuzungumza kwa sasa.”

Ends.

error: Content is protected !!