January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kahangwa apewa fomu ya urais NCCR-Mageuzi

Faustin Sungura (katikati), Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi NCCR – Mageuzi akimkabidhi fomu ya kugombea urais mwakilishi wa Dk. George Kahangwa, Mawazo Athanas (kushoto) ambaye ni Katibu Mkuu Vijana Taifa wa chama hicho.

Spread the love

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimemkabidhi, Dk. George Kahangwa, Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa chama hicho, fomu ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Anaandika Pendo Omary… (endelea).

Fomu hiyo ambayo imelipiwa Sh. milioni moja na imekabidhiwa na Faustin Sungura- Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi ya chama hicho huku Dk. Kahangwa akiwakilishwa na Mawazo Athanas, Katibu Mkuu Vijana Taifa.

Machi mwaka huu, Mwenyekiti wa Kitengo cha vijana wa NCCR- Mageuzi, Deo Meck, aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, kuwa Kahagwa, ndiye aliyependekezwa na vijana kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais.

Akizungumza kabla ya kukabidhi fomu hiyo, Sungura amesema “leo chama kinafungua rasmi pazia la wagombea ndani ya chama kwa kukabidhi fomu ya urais kwa ndugu George Lenarld Kahangwa”.

“Kahangwa ni mtoto wa saba katika familia ya mwalimu Gabriel Kahangwa na Anastazia Kakunyeta. Ni baba wa familia ya mke mmoja na watoto wawili. Ni mwanachama aliyelelewa katika maadili na itikadi ya chama chetu,” amesema.

Sungura amesema Kahagwa alizaliwa 5 Mai 1969 na chama hicho hakina mashaka yoyote na uwezo wake wa kuwatumikia watanzania kwa nafasi nyeti.

“Pamoja na pazia la wagombea urais ndani ya chama kufunguliwa rasmi, chama kinawaomba watanzania kujiandaa kisaikolojia kupokea mgombea urais wa Tanzania Bara au Zanzibar ama Waziri Mkuu kupitia Ukawa,” amesema Sungura.

Ukawa ni Umoja wa Katiba ya Wananchi, unaovishirikisha vyama vya Chadema, NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League Democrat (NLD). 

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo kwa niaba ya Dk.Kahagwa, Athanas amesema “Machi tuliitisha mkutano na waandishi wa habari. Tulieleza kuhusu kumuomba kugombea urais kupitia chama hiki. Baada ya kumuona alitukubalia rasmi. Tumechanga fedha na leo tumemchukulia fomu.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi ndani ya chama hicho, 1 Aprili hadi 15 Juni mwaka huu, ni kipindi cha kuchukua na kurejesha fomu za wagombea urais.

Aidha, 30 Aprili hadi 15 Juni, ni kuchukua na kurejesha fomu za wagombea wa udiwani. 15 Juni hadi 20 Julai, watachukua na kurejesha fomu wagombea uwakilishi/ubunge.

Kumbukumbu za chama hicho zinaonesha mwaka 1995, Augustin Mrema ndiye aliyekuwa mgombea urais akifuatiwa na marehemu Dk. Sengondo Mvungi mwaka 2005 na Hashim Rungwe mwaka 2010.

error: Content is protected !!