July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kagame tuhumani kumng’oa Nkurunziza

Spread the love

SERIKALI ya Rwanda inatajwa kuendesha mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi wa Burundi waliopo nchini mwake kwa lengo la kumuondoa madarakani Pierre Nkurunzinza, Rais wa Burundi. Shirika la Utangazaji la Reuter limeripoti.

Reuter limenakili Ripoti ya siri ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kwenye ripoti hiyo, inailaumu Serikali ya Rais Paul Kagame kuendesha mafunzo hayo.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na wataalamu wanaoangalia vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), imeonwa na shirika hilo Jumatano wiki iliyopita.

Taarifa kwenye ripoti hiyo imeeleza kuwepo kwa ushahidi mbalimbali na mzito unaoihusisha Serikali ya Rwanda kuingilia mambo ya ndani ya Burundi hivyo kuchochea hofu na vurugu za kisiasa ambazo zinaweza kuongeza machafuko.

Taarifa hiyo ni mjumuisho wa taarifa kutoka kwenye makundi mbalimbali ya waasi, waliowaambia maofisa hao wanaoshughulikia vikwazo kuwa, mafunzo hayo yanamekuwa yakifanyika katika kambi zilizopo Rwanda.

Hatua ya Nkurunzinza kugombea urais kwa muhula wa tatu imechochea kuibuka kwa machafuko tangu Aprili mwaka jana baada ya kutangaza kuwania nafasi hiyo.

Kwenye ripoti hiyo, maofisa hao wamesema, wamezungumza na wapiganaji 18 wa Burundi waliopo DRC katika Jimbo la Kivu.

“Wapiganaji hao waliwaambia maofisa kuwa wamepata mafunzo katika kambi ya wakimbizi ya Mahama huko Mashariki mwa Rwanda, mafunzo yaliyofanyika kati ya Mei na Juni 2015.

“Mafunzo hayo yalikuwa ni ya miezi miwili na yalitolewa na maofisa wa Jeshi wa Rwanda,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. Ripoti hiyo imeeleza, miongoni mwa wapiganaji waliofundishwa na Maofisa wa Kijeshi wa Rwanda wana umri wa miaka sita.

Na kwamba, miongoni mwa mafundisho waliyopewa wakimbizi hao ni pamoja na mbinu za kijeshi, matumizi ya bunduki, mabomu ya kutupa kwa mkono, mabomu ya kujeruhi askari, mabomu ya kuaribu magari na vifaru, mabomu ya kurushwa na roketi na silaha nyingine.

Wapiganaji hao wamesema, kuna angalau vikundi vinne vyenye jumla ya wapiganaji 100 waliopata mafunzo kwenye kambi za porini huko Rwanda.

“Walisafirishwa wakiwa ndani ya Rwanda wakiwekwa nyuma ya magari ya kijeshi na muda wote walisindikizwa na wanajeshi wa Rwanda,” Ripoti hiyo imeeleza na kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kumuondoa Nkurunzinza madarakani.

Eugene Gasana, Balozi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda amekanusha ripoti hiyo kadri ilivyonukuliwa na Reuters.

“Hii inazorotesha, kinachoelezwa na maofisa hawa wa UN kimepitiliza majukumu yao ya kuichunguza Burundi.”

Desemba mwaka jana Burundi iliituhumu Rwanda kuwa inaunga mkono waasi hao waliokuwa wakimbizi ndani ya ardhi Burundi. Tuhuma hizi zilipingwa vikali na Rais Kagame kuwa “tuhuma hizo ni za kitoto.”

Maofisa wa Baraza la Ulinzi la Umoja wa Mataifa walifanya safari kwenda Burundi Januari mwaka huu ikiwa ni safari yao ya pili katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.

Umoja wa Mataifa unakisia kuwa, watu 439 na zaidi wamepoteza maisha, pia zaidi ya watu 240,000 wamekimbia nje ya Burundi.

error: Content is protected !!