RAIS wa Rwanda, Paul Kagame, amewafuta kazi Meja Jenerali Aloys Muganga, Brigedia Jenerali Francis Mutiganda, pamoja na maafisa wengine 14 wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Aidha, kiongozi huyo wa muda mrefu nchini Rwanda, ameidhinisha kutimuliwa kwa wanajeshi wengine 116 wenye nyadhifa mbalimbali na kuidhinisha kusitishwa kwa mikataba ya utumishi za wanajeshi 112 wa vyeo vingine, kwa mujibu wa taarifa ya RDF.
Taarifa hiyo haikutoa sababu ya kufutwa kazi kwa wanajeshi hao 244, iliyotangazwa mapema jana Jumatano.
Meja Jenerali Muganga, ambaye hadi anafutwa kazi alikuwa kamanda wa kitengo cha kiufundi, ni mhitimu wa Chuo cha Vita cha Marekani na aliwahi kuwa kamanda wa vikosi vya akiba vya Rwanda kutoka mwaka 2018 hadi 2019.
Brigedia Jenerali Mutiganda alikuwa mkuu wa usalama wa nje katika Huduma za Kitaifa za Ujasusi (NISS) hadi 2018 wakati Rais Kagame alipomhamisha tena katika makao makuu ya RDF katika mji mkuu Kigali.
Mabadiliko haya yakuja siku moja baada ya Rais Kagame, kufanya mabadiliko makubwa ya maafisa wakuu wa kijeshi.
Aidha, mabadiliko ya kuwafuta kazi vigogo hao yamekuja wakati ambapo mvutano umeongezeka kati ya Rwanda na jirani yake wa magharibi – Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ukizidi kushika kasi.
Ni baada ya serikali mjini Kinshasa, kuituhumu Rwanda kuchochea uasi mwake kwa kuwasaidia kundi la waasi la M23.
Katika mabadiliko yaliyotangazwa juzi, Kagame alimteuwa waziri mpya wa mambo ya ndani, mkuu mpya wa kijeshi, pamoja na mkuu mpya wa ujasusi. Juvénal Marizamunda, alitangazwa kuwa waziri mpya wa ulinzi wa Rwanda.
Naye Luteni Jenerali Mubarakh Muganga, alikabidhiwa jukumu la kuwa mkuu mpya wa majeshi (RDF).
Bwana Marizamunda, ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa mkuu wa jeshi la Magereza, amechukua nafasi ya Meja Jenerali Albert Murasira.
Kwa upande wake, Luteni Jenerali Muganga, alichukua nafasi ya Jenerali Jean Bosco Kazura, aliyekuwa kamanda mkuu wa jeshi la ardhini.
Leave a comment