January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kafumu atetea “askari wa” Kagera

Mbunge wa Igunga, Dk. Dalali Kafumu

Spread the love

MBUNGE wa Igunga, Dk. Dalali Kafumu, ameibana Serikali ieleze ni lini itawalipa mafao askari walioshiriki vita ya Kagera, iliyokuwa na lengo la kumuondoa dikteta Nduli Idd Amini.

Amesema kuwa, askari hao ambao hivi sasa ni wastaafu wana kila sababu ya kulipwa kama ambavyo walilipwa wengine waliopigana vita hiyo.

Katika swali lake, Kafumu amesema “mwaka 1978, askari wengi wakiwemo kutoka JWTZ, Jeshi la Polisi na Magereza walishiriki vita ya Kagera. Mwaka 1979 baada ya ushindi askari hao walilipwa mafao ambayo hayakutosheleza kutokana na kazi waliyoifanya. Je, lini Serikali itawalipa?

Akijibu swali hilo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.Hussein Ali Mwinyi, ameliambia Bunge kuwa ni kweli katika kipindi hicho kuna askari ambao walipitia kupigana vita hiyo ambapo miongoni mwao kuna baadhi waliumia, kupata ulemavu na wengine kupoteza maisha na wengine walirudi salama.

Amesema askari hao ama familia zao walilipwa fedha stahiki kulingana na viwango vya wakati huo na kwamba sio kweli kuwa walilipwa mafao ambayo hayakutosheleza.

Akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyetaka kujua ni lini Serikali itawapa nyongeza ya fedha kama ilivyoahidi, Dk.Mwinyi amesema kwa wakati huo, askari wote waliostahili walilipwa na kwamba nyongeza iliyoahidiwa ni ya pensheni kwa wastaafu wote.

error: Content is protected !!