August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kafulila: Sintoisahau Clouds TV

Spread the love

YALIYOMKUTA David Kafulila, katika Studio za Kituo cha Utangazaji cha Televisheni ya Clouds, hatokisafau maishani mwake, anaandika Pendo Omary.

Ni kwa kuwa, alialikwa kuzungumzia masuala ya uchumi na baada ya kufika, aliandaliwa kama wageni wangine wanavyoandaliwa lakini ghafla wakamtosa.

Kafulila aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (2010-2015) amesema “sintoisahau siku hii.” Amesema alialikwa na chombo hicho cha habari kuzungumzia mwenendo wa uchumi nchini.

Ni kutokana na historia yake alipokuwa mbunge kwamba, alikuwa kinara kwenye Bunge la 10 baada ya kuibua ufisadi wa uchotwaji wa zaidi ya Sh. Bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hata hivyo Kafulila akiwa tayari ametayarishwa kwa kuvalishwa kipazasauti ili kuanza mjadala katika kipindi cha 360, ghafla aliombwa radhi kwamba “kuna maelekezo kutoka kwa mkurugenzi kuwa, kipindi kisirushwe.”

Akizungumza na MwanaHALISI Online leo baada ya kuondolewa katika studio za kituo hicho amesema “binafsi sikutarajia siku moja kukutwa na hali hii.

“Sikujua kama siku moja Tanzania itafika hatua hii. Nilijisikia vibaya kuvuliwa mice nikiwa tayari kwa mjadala lakini nilijua tatizo ni zaidi ya watangazaji.

“Nilitaka kuzungumzia kwa mapana anguko la sekta ya fedha na sekta binafsi na mazingira ya biashara na uwekezaji kwa ujumla na namna athari yake inavojitokeza kwenye kupunguza uwezo wa serikali kutoa huduma kama elimu, afya kwa mujibu wa ripoti mbalimbali.”

Aidha, Kafulila amesema anadhani kulikuwa na maelekezo ya ziada nje ya mfumo wa kituo hicho kwa sababu, haamini kama tangazo ambalo lilirushwa jana kutwa nzima pia leo asubuhi bila mkurugenzi kufahamu.

Na kwamba, hata kama angejua bado vipindi ni suala la wataalamu wa utangazaji.
“Sijui mmiliki alihofu nini kwangu. Hali ya uhuru wa vyombo hivi ni tete na kwa sheria ya habari inayokwenda kupitishwa bunge lijalo, vyombo vyote vitakuwa chini ya ulinzi wa dola na ndio mwisho wa uhuru wa vyombo hivi,” amesisitiza Kafulila.

error: Content is protected !!