January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kafulila: Serikali ya CCM ni “misheni town”

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila

Spread the love

DAVID Kafulila- Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), ameivaa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema imechafua taswira ya Tanzania nje ya nchi kutokana na kushindwa kudhibiti vitendo vya ufisadi. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Kwa mujibu wa Kafulila, Tanzania sasa inaogopeka kukopesheka kutokana na viongozi wake kuwa watu wa kupiga madili.

“Serikali ya CCM ni ya watu wa misheni town. Haiwezi kufanya lolote kudhibiti ufisadi. Nyie mlioko huko wenye nia ya kuisaidia nchi hii, Ukawa ndio mpango mzima, njooni huku,” amesema.

Kauli ya Kafulila ya maneno “kupiga madili” na “misheni town” ina maana kwamba viongozi wa juu katika Serikali ya CCM, wanashirikiana na watendaji mawizarani na asasi za serikali kupata mipango ya kufisidi uchumi wa Tanzania kupitia mikataba ya miradi ya maendeleo na ununuzi wa vifaa ndani ya serikali.

Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2015/16, Kafulila ameitaka serikali kuweka nguvu kujenga reli ya kisasa kwa sababu ndio usafiri rahisi, salama na wenye kubeba mizigo mingi kwa wakati.

Amegusia kashfa ya ununuzi wa mabehewa chakavu yaliyogharimu zaidi ya Sh. 203 bilioni, akisema ni zaidi ya kashfa ya zabuni tata ya Richmond ya mwaka 2008, akihoji inawezekanaje serikali inatoa fedha zote kabla ya kupokea mzigo ulionunuliwa.

Kuhusu usafiri wa anga, Kafulila amesema ni jambo la aibu nchi ndogo kama Rwanda ambayo ukubwa wake ni mara mbili kwa mkoa wa Kagera, ina ndege saba lakini Tanzania inayo moja, tena ya kukodi ambayo kila siku iko gereji.

error: Content is protected !!