July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kafulila apata tuzo ya kufichua Escrow

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila akipokea tuzo ya Utetezi wa Haki za Binadamu kutoka kwa THRD

Spread the love

DAVID Kafulila-Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), ametunukiwa tuzo na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRD), akiwa miongoni mwa watu watatu ambao wamefanya kazi katika mazingira magumu kwa lengo la kutetea haki mwaka 2014. Anaandika Pendo Omary …(endelea).

Pamoja na Kafulila, wengine ni aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la 201 akiwakilisha Zanzibar, Salma Said na Mkurugenzi wa Baraza la Wanawake Wafugaji kutoka Loliondo, Maanda Ngoitiko.

Akizungumza na MwanaHALISIOnline, Mratibu wa THRD, Onesmo Ole Ngurumwa amesema watu hao ni wale “waliofanya kazi ya kutetea haki za binadamu katika mazingira magumu huku wakitishiwa kuuwawa lakini kazi zao zimesaidia kuleta mabadiliko”.

“Nawasihi watu waendelee kupigania haki. Licha ya kwamba wanatishwa na hata wengine kuuwawa, wanapaswa kusimamia kile wanachokiamini ambacho ni haki,” amesema Olengurumwa

Ameongeza kuwa, maaadhimisho haya ni ya pili kufanyika Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2013.

Ametaka siku hii itambuliwe kimataifa na isiwe nchini tu, huku akisisitiza kwamba wanaofanya utetezi huo waangalie usalama wao katika harakati za kupigania haki za wengine.

Naye Ernest Sungura, Mkurugenzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), amesema katika kuelekea katika uchaguzi mkuu, wanahabari wanatakiwa kulindwa na vyombo vinavyoweza kudhamiria kuwakingia kifua kutokana na wao kuandika habari za uchunguzi ambazo mara kwa mara zimeonekana kugusa maslahi ya watu mbalimbali moja kwa moja.

Wawakilishi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya nchini na washauri wa masuala ya haki za binadamu katika nchi za Umoja wa Mataifa, wameeleza kuwa, kama Serikali haithamini haki za mtu mmoja mmoja ipo hatari kubwa ya kupoteza nguvu kazi ya taifa kwa jambo ambalo lingeweza kutatuliwa kwa njia rahisi.

Balozi wa Jumuiya ya Ulaya chini, Filberto Sebrregondi, amesema umefika wakati wa kila mwananchi kutambua kuwa wimbi la kuminywa haki za watu wasio na uwezo linakuwa kwa kasi nchini, licha ya kubainisha kwamba amefurahishwa kwa namna washiriki walivyoonyesha ushirikiano kwa mwamvuli wa mitandao hiyo ya kutetea haki za binadamu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo-Bisimba, akiongea katika maadhimisho hayo, alisisitiza kwamba haki za binadamu ndizo zinazowafanya wanadamu waishi na kwamba mtu yeyote asipofanya utetezi wa haki za binadamu anataka ubinadamu wa wengine uishie njia panda.

Kwa upande wake, Kafulia ambaye amepewa tuzo hiyo kwa kuibua bungeni kashfa ya ufisadi wa Sh. 306 bilioni katika akaunti ya Tegeta Escrow, ameliambia MwanaHALISIOnline kuwa “tuzo hii imenipa ujasiri zaidi katika kusimamia maslahi ya taifa katika vita vya ufisadi. Inaonesha katika mapambano haya sipo peke yangu”.

“Ni mara yangu ya kwanza kuingia bungeni. Tena nikiwa kijana. Hakuna mbunge aliyewahi kukabidhiwa tuzo hii hasa kwa kazi niliyoifanya ya kuibua ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow. Inaonesha vijana tunaweza. Japo ilikuwa ni kazi hatari na wakati mwingine nilitishiwa maisha yangu,” amesema Kafulila.

Ameupongeza mtanda wa THRD na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa ushauri wa kisheria waliompa wakati akitoa ushahidi wa ufisadi wake kwenye mamlaka za uchunguzi na hata alipofunguliwa kesi na Seth Herbinder Singh, mmoja wa wanufaika wa fedha za Escrow.

Naye Salma Said, alitishiwa maisha baada ya kuonesha msimamo wake hadharani wa kupinga Rasimu ya Katiba inayopendekezwa akisema “ni kinyume na maoni yalitotolewa na wananchi” huku Ngoitiko akiwa ni mtetezi wa haki za binadamu vijijini hasa wafugaji walionyang’anywa maeneo yao Loliondo mkoani Arusha.

Tuzo hizo zimejumuisha cheti cha kutambua mchango wa kupigania haki na ngao ambayo ni alama ya ushujaa.

Maadhimisho hayo yameenda sambamba na maonyesho ya watetezi hao, ambao ni Kampuni ya Jamii Media (Wamiliki wa mitandao maarufu ya kijamii nchini ya FikraPevu.com na JamiiForums, TGNP Mtandao, TAMWA, LHRC, HAKI ARDHI INSTITUTE, JUKWAA LA KATIBA, TAWLA, SIKIKA, ZLSC, TAS, TACOSODE, TANLAP, LEAT,Human Rights Comission, TVVA, Haki Catalyst, German Foundation, German Embasy, SANA, na CESOPE.

error: Content is protected !!