December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kafulila akamilisha sharti la mahakama

Spread the love

ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, jana alitekeleza agizo la Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa kutoa Sh. 7,500,000 milioni ili kusikilizwa kesi yake. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Wakati akifungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Husna Mwilima katika jimbo hilo, mahakama hiyo ilimtaka Kafulila atoe Sh. 15 milioni kama dhamana ya kusikilizwa kesi hiyo yenye washitakiwa watatu.

Kafulila anadai kushinda uchaguzi huo na kwamba, anachohitaji ni kuomba mahakama imvue ubunge Husna na kumtangaza yeye kuwa mshindi.

Awali, Jaji Leila Mgonya anayesikiliza kesi hiyo alimtaka Kafulila kulipa dhamana ya Sh. 5,000,000 kwa kila mshitakiwa na kufanya Sh. 15 milioni kwa washitakiwa watatu.

Kafulila kupitia kwa wakili wake Emmanual Msya, aliwasilisha ombi la kupunguziwa kiasi hicho cha fedha katika mahakama hiyo na kuwa Sh. milioni moja kama dhamana kwa kila mlalamikiwa.

Sababu zilizotolewa na wakili huyo ni kwamba, Kafulila hakuwa na uwezo wa kulipa Sh. 15 milioni zilizotajwa awali kwa mujibu wa sheria ya kesi za uchaguzi.

Akizungumza na gazeti hili leo kwa njia ya simu baada ya uamuzi huo kutolewa jana mahakamani hapo, Kafulila amesema ameridhika na uamuzi huo wa mahakama na amelipa kiasi hicho cha fedha ili kesi yake ya msingi iweze kusikilizwa na kutolewa hukumu.

Kafulila amesema, kwa mujibu wa jaji washitakiwa watajibu madai hayo ndani ya siku 21 ambapo kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa mfulizo kuanzia januari mwakani na kwamba, itasikilizwa ndani ya siku 90 na kutolewa hukumu.

“Jaji akitoa hukumu na nisiporidhishwa, nitakata rufaa na kuipeleka mahakama za juu japo sitarajii hayo kutokea. Ninaimani uamuzi wa mahakama utakuwa wa haki kwani nina uhakika wa kushinda kesi yangu,” amesema Kafulila.

error: Content is protected !!