January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kafulila aibua ufisadi wa mabehewa TRL

Waziri Mkuu Mizengo Pinda na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe (nyuma) wakikagua moja ya mabehewa mapya ya TRL

Waziri Mkuu Mizengo Pinda na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe (nyuma) wakikagua moja ya mabehewa mapya ya TRL

Spread the love

DAVID Kafulila-Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) ameweka hadharani udhaifu ulioainiswa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), katika michakato ya zabuni mbili za manunuzi ya mabehewa. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Zabuni hizo ni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 ya ununuzi wa mabehewa 25 ya mizigo (supply of New Ballast Hopper Bogie Wagons).

Zabuni ya pili ni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/014 ya ununuzi wa mabehewa ya mizigo 274 (supply 274 New Goods Wagons).

Kafulila ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda na Biashara, ndiye muasisi wa kashfa ya ufisadi wa sh. 306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow  ambao umeng’oa mawaziri wawili na Mwanasheria Mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema taarifa ya awali iliyotolewa Machi mwaka huu na PPRA kuhusu uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa uliofanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL), umebaini upungufu ufuatao;

Kanuni na taratibu chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 (ambayo ilifutwa na Sheria Namba 7 ya mwaka 2011) zilizotumika katika ununuzi huo.

“PPRA imebaini kuwa TRL waliingia mkataba na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited ya India bila kujiridhisha kuhusu uwezo wa kampuni hiyo kama ilivyoelekezwa kwenye nyaraka za zabuni,” amesema Kafulila.

Hivyo, TRL ilikiuka kifungu cha 53 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma na matakwa ya nyaraka za zabuni ambazo zilitaka uchunguzi huo ufanyike.

Aidha, uchunguzi umebaini kuwa zabuni hizi zilitangazwa kwenye magazeti ya ndani peke yake bila kutangazwa kwenye gazeti moja la kimataifa kama inavyoelekezwa kwenye nyongeza ya kwanza ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.

“Hii inapunguza ushiriki wa kampuni za nje kwa kutopata taarifa ya tangazo la zabuni hiyo,” inasomeka sehemu ya taarifa ya PPRA.

Aidha, uchugunguzi umebainisha pia kuwa uandaaji wa mahitaji (specifications), uliofanywa na Idara Hitaji kuhusu mabehewa yaliyokuwa yanahitajika ulikuwa dhaifu.

Hii imedhihirika kutokana na kamati nne za ukaguzi kutumwa India kwa nyakati tofauti kukagua utengenezaji wa mabehewa hayo na kuendelea kutolewa mapendekezo ya marekebisho ya mahitaji ya mabehewa hayo.

Taarifa hiyo inasomeka “utekelezaji wa mikataba yote miwili TRL walichelewa kutekeleza maombi ya malipo ya awali na iliathiri muda wa utekelezaji wa mikataba hiyo”.

Pia, PPRA imebaini menejimenti ya TRL haikuwa makini kushughulikia maombi ya kuongezewa muda yaliyokuwa yanawasilishwa na kampuni ya Hindusthan Engineering Limited.

Kwa mfano; katika mkataba wa zabuni PA/133/2012-13/ME/G/OE/014, kampuni hiyo iliwasilisha maombi 13 Mai, 2014 ya kuomba kuongezewa muda wa mkataba hadi 14 Disemba, 2014.

 Maombi hayo yaliidhinishwa na TRL 16 Mai, 2014 na muda wa mkataba uliongezwa hadi 30 Septemba 2014.

“Kwa hali ya nchi yetu ilipofika ni lazima hii taarifa itoke, watu wajue kinachoendelea. Hivyo kwa taarifa ya awali ya PPRA ni lazima hatua zichukuliwe na mamlaka husika,” ameongeza Kafulila.

Mkataba huo ulisainiwa kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India 21 Machi 2013, wenye thamani ya Dola za Kimarekani 2,561,187.50.

Zabuni hii iligawanyika katika makundi matatu: kundi la kwanza mabehewa ya mizigo 174 (Covered Large Bogie Wagons), kundi la pili mabehewa 50 (Petro Tank Bogie Wagons) na kundi la tatu mabehewa 50 (Container Carrier Wagons).

Mkataba wa ununuzi wa mabehewa 274 ulisainiwa kati ya TRL na kampuni ya Hindusthan Enginneering and Industries Limited ya india kwa thamani ya jumala ya Dola za Kimarekani 28,487,500.

PPRA inafanya uchunguzi huo kwa kuangalia iwapo taratibu za manunuzi zilizoainishwa katika Sheria na Kanuni za Manunuzi ya Umma zilizingatiwa; utekelezaji wa mkataba ulizingatia masharti na taratibu zilizoaninishwa kwenye mkataba;

Ilichunguza iwapo mabehewa yaliyopokelewa ni mapya au yametumika na itatoa mapendekezo ya kuboresha utendaji kazi wa TRL au hatua za kuchukua dhidi ya watakaobainika kuhusika katika ukiukwaji wa Sheria, kanuni na Miongozo ya Manunuzi ya Umma.

error: Content is protected !!