September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kada CCM apinga ‘papara’ za kuhamia Dodoma

Spread the love

FESTO Mgina, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ameshangazwa na ‘ukurupukaji’ wa Serikali kutaka kuhamia katika Mkoa wa Dodoma pasipo kufanya maandalizi ya msingi, anaandika Charles William.

Mgina ambaye pia ni Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata ya Mninga, Wilaya ya Mufindi inayojumuisha majimbo ya Mufindi Kaskazini, Mufindi Kusini na Mafinga Mjini, amesema suala la kuhamia Dodoma halihitaji papara kama baadhi ya mawaziri wanavyotangaza.

“Mwalimu Julius Nyerere aliasisi suala hili kwa nia njema na ni vyema kuliendeleza jambo hili, lakini siyo kwa haraka au ghafla kama inavyoelezwa kwa sasa. Kuhamia Dodoma kunahitaji serikali na watendaji kujipanga zaidi,” amesema na kuongeza;

“Baadhi ya mawaziri wanadai, watahamia ndani ya miezi miwili. Binafsi najiuliza watauza kwanza majengo ya Dar ndiyo wapate fedha ya kujenga Dodoma? Na kama ni hivyo watajenga ndani ya muda gani? Watajenga kwa ubora?.”

Mgina alikuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Ebony Fm cha mkoani Iringa mapema leo asubuhi, ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia utendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Mufindi pamoja na changamoto zake.

Ameeleza kasi ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo, pamoja na utendaji unaozingatia misingi ya Sheria na Utawala bora uliosababisha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuipa hati safi halmashauri hiyo.

Suala la kuhamia Dodoma kwa ghafla limekuwa likikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa watu wa kada mbalimbali tangu kutangazwa kwake na Rais John Magufuli, 23 Julai mwaka huu.

25 Julai mwaka huu, Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu alinukuliwa katika Sikukuu ya Mashujaa akisema kuwa, “Nimeagiza nyumba yangu ikamilishwe na Septemba nitahamia Dodoma na baada ya mimi kuhamia mawaziri wote hakuna atakayetakiwa kubaki Dar.”

Kuhama kwa mawaziri, kutalazimu pia kuhama kwa watendaji wa wizara zote wakiwemo wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali pamoja na familia zao, jambo ambalo katika mantiki ya kawaida haliwezi kufanikiwa ndani ya kipindi cha miezi miwili lakini pia, hakuna bajeti iliyopitishwa kutekeleza suala hilo.

 

error: Content is protected !!