Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Tangulizi Mwandishi wa habari Kabendera, amwangukia Rais Magufuli 
Tangulizi

Mwandishi wa habari Kabendera, amwangukia Rais Magufuli 

Mwanahabari Erick Kabendera akiingia mahakamani Kisutu
Spread the love

ERICK Kabendera, mwandishi wa habari za uchunguzi, mtafiti na mshauri wa kimataifa wa masuala ya siasa, habari na uchumi, ameomba msamaha kwa Rais John Magufuli, ili kuweza kuwa huru. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).

Kabendera, anayezuiliwa kwenye gereza kuu la Segerea, jijini Dar es Salaam, anakabiliwa na mashitaka matatu ya uhalifu, likiwamo la utakatishaji fedha.

Wakili wa mshitakiwa huyo, Jebra Kambole, ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano, tarehe 1 Oktoba 2019, kuwa mteja wake Kabendera ameomba msamaha huo ili kuweza kuwa huru na kuendelea na shughuli zake nyingine.

Kwa mujibu wa Jebra, “Kabendera amemuomba radhi Rais Magufuli, akieleza kwamba kama katika utekelezaji wa majukumu yake ya uanahabari, kuna eneo alifanya makosa au aliteleza, amsamehe ili aweze huru.”

Mwandishi huyo mahiri wa habarialijulikana kuwa anashikiliwa na jeshi la Polisi, tarehe 29 Julai 2019, kufuatia Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kukiri kuwa jeshi lake, linamshikilia Kabendera kwa madai ya “utata wa uraia wake.”

 

Kauli ya Kabendera ilifuatia kuibuka kwa taharuki miongoni mwa jamii zilizokuwa zikieleza kuwa mwandishi huyo alichukuliwa nyumbani kwake, maeneo ya Mbweni jijini Dar es Salaam na wanaoitwa “watu wasiojulikana.”

 

Mambosasa alidai kuwa hatua ya jeshi hilo kuvamia nyumbani kwa Kabendera na kumkamata, imetokana na kile alichokiita, “kukaidi amri ya jeshi la Polisi.”

Maofisa wa jeshi la Polisi, walivamia nyumbani kwa Kabendera, tarehe 26 Julai 2019 na kumchukua kwa nguvu na kumzunguusha kwenye vituo kadhaa vya polisi.

Mambosasa aliutangazia umma kuwa “tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu, kwamba mwandishi huyu wa habari alitekwa na watu wasiojulikana. Ukweli ni kuwa hajatekwa. Amekamatwa na jeshi la polisi na sasa tunamshikilia kutokana na utata wa uraia wake.

 

Amesema, “tulimuita kwa njia ya kawaida ili kufanya naye mahojiano. Lakini akakataa kuja. Hivyo tukaamua kumkamata kwa kutumia taratibu zetu na sheria nyingine za nchi.”

 

Amesema, Jeshi la Polisi linamhoji Kabendera kwa kuwa lina mashaka na uraia wake. Amedai mwandishi huyo awali aliandikiwa barua ya wito kufika polisi kwa ajili ya mahojiano lakini hakuitikia wito huo.

Hata hivyo, wiki moja baadaye alipandishwa kizimbani akituhumiwa kuongoza kundi la uhalifu kwa madhumuni ya kujipatia faida au manufaa mengine; kutokulipa kodi inayokadiriwa kufikia zaidi ya Sh. 173.24 milioni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na utakatishaji wa kiasi cha Sh. 173.24 milioni.

Wakili Jebra ameeleza katika taarifa yake mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Augostino Rwizile, kuwa “…lakini jambo la msingi, ujumbe wa Erick kwa mheshimiwa rais ni kwamba kama katika kutimiza wajibu wake kama mwandishi wa habari kuna eneo alikosea au alitereza, tuombe radhi kwa niaba yake, watoto na familia yake kwa ujumla.”

Aidha, Jebra amesema, Kabendera yuko tayari kufanya jambo lolote, ili kulinda uhuru na usalama wake.

Amesema, “tumuombe radhi kwa nafasi yetu, tuseme wazi kama atapata ujumbe huu, aweze kuufanyia kazi. Hilo jambo kama ataona kuna mahali  Erick anatakiwa kufanya jambo lolote, si tuko tayari kufanya, ili kulinda uhuru wake na kupata uhuru kuwa nje kama raia wa kawaida.”

Erick Kabendera, ni mwandishi wa habari za uchunguzi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa; uchumi na usalama wa kikanda. Anaripoti katika magazeti mbalimbali, likiwamo Africa Confidential linalochapishwa nchini Uingereza. Aliwahi kuhojiwa uraia wake miaka 10 iliyopita, lakini polisi walisema wamejiridhisha kuwa hakuwa na shida.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

‘Aliyemtonya’ Lissu kuhusu rushwa arejea madarakani

Spread the loveMwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Iringa, William Mungai...

Habari za SiasaTangulizi

Wabunge wacharuka kukatika kwa umeme

Spread the loveTATIZO la kukatika kwa umeme kila mara katika maeneo mbalimbali...

Habari za SiasaTangulizi

Watu 1,673 wamchangia Lissu Sh. 20 milioni kununua gari

Spread the loveWATU 1,673 wamechanga fedha zaidi ya Sh. 20 milioni kwa...

Habari MchanganyikoTangulizi

11 wafariki dunia baada ya mtambo wa Kiwanda cha Mtibwa Sugar kupasuka

Spread the loveWATU 11 wamefariki dunia huku watatu wakijeruhiwa katika ajali ya...

error: Content is protected !!