September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kabendera aimwagia chozi mahakama

Spread the love

HATIMA ya mwandishi wa habari nchini, Erick Kabendera, kushiriki msiba wa mama yake mzazi, Mwalimu Verdiana Mujwahuzi, itajulikana muda mfupi kutoka sasa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Kabendera anayekabiliwa na mashitaka matatu ya ukwepaji kodi ya Sh. 173 milioni; utakatishaji fedha na madai ya kujihusisha na magenge ya uhalifu, anazuiliwa katika gereza kuu la mahabusu, Segerea jijiji Dar es Salaam.

Akiwasilisha maombi ya kutaka Kabendera ashiriki ibada ya kumuaga mama yake, mmoja wa mawakili wake, Jebra Kambole amesema, ni muhimu kwa mshitakiwa huyo kupewa ruhusa hiyo ya kushiriki msiba wa mama yake.

“…tunaiomba mahakama imruhusu Kabendera akatoe heshima za mwisho kwenye mwili wa mama yake mzazi. Hili ni takwa la kisheria na Jamhuri (upande wa mashitaka), haitaathirika kwa lolote kwa mahakama kutoa ruhusa ya aina hiyo,” ameeleza Jebra.

Ameongeza: “mshitakiwa mwenyewe atakuwa chini ya ulinzi, na ibada itakuwa mchana kanisani; na kwamba kunakofanyika ibada ya mazishi huko Temeke siyo mbali na gerezani anakohifadhiwa Kabendera.”

Mama mzazi wa Kabendera, alifariki dunia juzi tarehe 31 Desemba 2019, jijini Dar es Salaam. Mwili wake unatarajiwa kusafirishwa kesho kupele Bukoba, mkoani Kagera.

Mwandishi huyo wa habari alisababisha mamia ya watu waliokuwapo mahakamani, kujawa na huzuni, baada ya kumwaga chozi mbele ya halaiki.

Akiongea mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, Janeth Mtenga, leo tarehe 2 Januari 2020,Jebra alisema, ni ubinadamu na takwa la kisheria, kumruhusu mshitakiwa kushiriki msiba wa mmoja wa wazazi wake, mke wake ama mtoto wake.

Hata hivyo, maombi hayo, yamepingwa na upande wa Jamhuri, kwa maelezo kuwa mahakama haina uwezo wa kusikiliza ombi hilo.

“Hata sisi tuna masikitiko makubwa na tunampa pole nyingi Kabendera kwa kufiwa na mama yake mzazi. Lakini maombi haya yapo mahakamani kinyume na sheria na hayawezi kutekelezeka,” ameeleza Wankyo Simon, wakili mkuu wa serikali akipinga ombi la Kabendera.

Alisema, isifungwe mikono kwa maombi yaliyowasilishwa ya kutaka kushiriki msiba, “mahakama hii haina mamlaka hayo.”

Kutokana na mabishano hayo yaliyoibuka, mahakama imeamua kuhairisha shauri hilo hadi baadaye ambako itatoa uamuzi wa iwapo Kabendera aruhusiwe kushiriki msiba wa mama yake akiwa chini ya ulinzi ama hataruhusiwa.

MwanaHALISI Online, linaendelea kupinga kambi mahakamani kufuatilia shauri hilo ili kuujulisha umma.

 

error: Content is protected !!