June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JWTZ yathibitisha vifo vya askari wake

Mkuu wa Majeshi wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange

Spread the love

JESHI la Wananchi Tanzania (JWTZ), limethibitisha vifo vya askari wake wawili vilivyotokea 5 Mei mwaka huu, saa 12:30 jioni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Anaandika Pendo Omary (endelea).

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo, Kurugenzi ya Habari na Mahusiano Makao Makuu ya Jeshi, Upanga, jijini Dar es Salaam inasema “askari hao waliuwawa baada ya gari lao kushambuliwa na kikundi kinachodhaniwa kuwa cha waasi wa ADF wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani DRC.”

Askari hao waliouwawa ni miongoni wa kikundi cha wanajeshi 46 waliokuwa katika jukumu hilo chini ya majeshi ya Umoja wa Mataifa.

“Awali kikundi hicho kilisafiri kwa ndege toka mji wa Abralose kuelekea katika mji wa Mavivi. Baada ya kufika katika mji wa mavivi, msafara huo ulielekea katika mji wa Mayimayo kwa njia ya barabara wakitumia magari ya kijeshi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo inasema “wakiwa njiani kuelekea katika mji wa Mayimayo, ndipo msafara wao ulipovamiwa na kikundi kinachodhaniwa kuwa cha waasi wa ADF na magari waliyokuwa wakisafiria walishambuliwa kwa silaha za kivita ambapo gari moja liliteketezwa na kusababisha vifo vya askari wawili papo hapo na wengine 16 kujeruhiwa”.

“Majeruhi hao 16 walipelekwa hospitali kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

error: Content is protected !!