January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JWTZ, Polisi wadaiwa sugu Tanesco

Spread the love

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Mwanza, limezilalamikia Taasisi za Serikali ikiwemo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambazo zimekuwa sugu katika ulipaji wa ankara ya umeme kitendo kinachosababisha ukusanyaji mdogo wa kodi. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa Tanesco mkoa wa Mwanza, Gerson Manase, wakati akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa Tanesco kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, hadi kufikia Oktoba mwaka huu.

Manase amesema kuwa Taasisi za Serikali zimekuwa sugu katika ulipaji wa ankara ya umeme kwa kutumia mgogo wa Serikali huku Tanesco ikiendelea kupata wakati mgumu wa utoaji huduma kwa wananchi.

Manase amesema Tanesco mkoa wa Mwanza inahudumia jumla ya wateja 90,925 kati ya hao 81,487 wanatumia mita za luku na 9,438 wanatumia mita za malipo, ambapo makusanyo kwa mwezi ni Sh. 6.4 bilioni.

Amesema licha ya kukusanya fedha hizo kwa mwezi bado wanakabiliwa na tatizo la watumiaji wa umeme kushindwa kulipa ankara zao kwani mpaka sasa wanazidai taasisi za Serikali na watu wengine Sh. 3 bilioni.

Hata hivyo alizitaja Taasisi za Serikali zinazodaiwa na Tanesco kuwa ni Jeshi la Wananchi Tanzania (TPDF) Sh. 809, 617 milioni, jeshi la Polisi, Sh. 515, 660, Magereza, Sh. 608, 306 na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) Sh. 347759.

“Mkuu wa mkoa (Magesa Mulongo) tunapata wakati mgumu sana kuzidai hizi taasisi za umma hususani TPDF na Polisi tunapoenda kuwadai na kuwaomba tuwafungie Luku, hawakubali sasa hali hii imekuwa ngumu,” amesema Manase.

Aidha amesema Tanesco inakabiliwa na tatizo la uchakavu wa vitendea kazi, uchakavu wa miundombinu ya usambazaji umeme, wizi wa nyaya na nguzo, madeni katika taasisi na wizi wa umeme kwa wateja unaofanywa na wateja.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, aliwataka wafanyakazi wa Tanesco kufanya kazi kwa bidii kwani shirika hilo limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwa kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mulongo amesema watu milioni 2.9 katika mkoa wa Mwanza wanahitaji huduma ya umeme lakini watumishi wachache ambao ni wazembe katika kuwatumikia wananchi wameonekana kikwazo kwa Taifa.

“Jamii inahitaji utumishi wa dhati na wanafahamu kibuli cha binadamu na watumishi wao, kama mtashindwa kufanya kazi kwa dhati itakula kwenu kwa Serikali hii wengi wenu mtakuwa nje ya mfumo wa ajira,” amesema Mulongo.

error: Content is protected !!