August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JUVICUF yalaani fujo Zanzibar

Spread the love

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Wananchi CUF (JUVICUF) umelaani matukio ya kikatili yanayoendelea kufanyika Zanzibar, anaadika Regina Mkonde.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Zanzibar, Mahmoud Mahinda, Katibu Mtendaji JUVICUF amesema kuwa matendo hayo yamewafanya wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hususan jeshi la polisi.

“JUVICUF tunalaani vikali vitendo hivyo vya hujuma vinavyoshamiri kila uchao katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar na inaichukulia hatua hii ya vyombo vya Ulinzi na Usalama, kukiuka taratibu zake za utendaji na kutekeleza uhuni dhidi ya raia wanyonge,” amesema.

Amesema kuwa unyama wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, yanadhihirika katika matukio ya hivi karibuni yaliyofanywa na askari wa jeshi la Polisi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Zanzibar.

“Kwa mfano, usiku wa tarehe 19 Juni, 2016 askari wa Jeshi hilo lilivamia kisiwa cha Mtambwe na kuwashambulia raia wa kisiwa hicho kwa mfululizo wa mabomu ya machozi usiku kucha,” amesema.

Aidha, amesema JUVICUF inamhakikishia Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia likuwa mgombea urais visiwani humo kwamba utaendelea kupigania haki yao.

“JUVICUF tunamhakikishia Maalim Seif Sharif Hamad kutumia ushawishi wetu tulionao kwa idadi kubwa ya vijana wa nchi hii kupigania haki zetu na za wazanzibari wenzetu licha ya kuwepo kila aina ya njama za kutufunga midomo zinazofanywa na watawala waovu kwa kuwatumia vibaraka wao walio katika maeneo na mamlaka mbali mbali za nchi yetu,” amesema.

Mahinda amesema JUVICUF haitotetereka wala haitokubali kurejeshwa nyuma kwa vitimbi vya watawala waovu vyenye lengo la kuzima sauti na madai dhidi ya haki zao.

Na kwamba badala yake, JUVICUF itaunganisha nguvu za vijana madhulumu wa Zanzibar na kutumia ari na nguvu zao kuhakikisha waliyemuita mtawala muovu anang’oka katika khatamu za Dola ya Zanzibar kwa kutumia njia za kidemokrasia zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria za nchi.

“Msimamo huu wa JUVICUF hautokani na khulka ya ubishi, ubabe, ama kibri kinachotokana na nguvu, bali silka ya uzalendo wa kuitetea nchi yetu na kupigania haki zetu za kiraia zilizoorodheshwa katika Katiba yetu,” amesema.

 

 

error: Content is protected !!