July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jumaa atatua mgogoro wa ardhi Kibaha

Spread the love

SERIKALI imetakiwa kuwafafanulia wakulima wa kilimo cha muda mfupi wanaotumia bonde la Kiwalani, wilayani Kibaha, kuhusu mradi unaotarajiwa kufanyika katika bonde hilo na umiliki halali wa mashamba hayo. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Bonde hilo lililopo kati ya Ruvu Darajani na Mlandizi ndani ya jimbo la Kibaha Vijijini ambalo linatumiwa hasa na wakulima wa mpunga, limekuwa na sintofahamu baada ya wananchi kulalamikia serikali kuwa inawadhurumu mashamba yao hayo kwa kuwasimamisha kufanya shughuli za kilimo.

Eneo la Kiwalani linadaiwa kuwa ni la serikali kwa miaka zaidi ya 60 iliyopita ambapo iliwaachia wananchi wa maeneo ya karibu kwa ajili ya kufanya kilimo cha muda mfupi kwakuwa linampango wa kuendelezwa.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mbunge wa Jimbo hilo, Hamoud Jumaa amesema kuwa kwa taarifa alizonazo, eneo hilo ni la serikali na si mtu binafsi hivyo serikali inapohitaji kuliendeleza eneo hilo ni jambo lisilozuilika.

Hamoud amesema kuwa jambo muhimu ambalo halijafanyika ni serikali kutotoa taarifa za kina kuhusu uendelezaji wa bonde hilo na kuwafafanulia wananchi kuwa si la mtu binafsi bali ni la serikali.

“Ninazo taarifa za mpango wa kuliendeleza bonde hilo kwa kuweka stendi ya kisasa, Soko na tayari halmashauri imeshaanza kupima maeneo, hayo yote ni juhudi za kutekeleza matakwa ya wananchi kuhusu mahitaji ya hiyo miundombinu,” amesema Hamoud nakuongeza:

“Kilichotokea hapa ni mahusiano baina ya wananchi na serikali siyo mazuri, hivyo kinachopaswa kufanyika ni serikali kuwa wawazi kwa wananchi wao wanaotumia bonde hilo kuwapa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kinachohitajika kufanywa.”

Akizungumza kwa kuonyesha kushangazwa na taarifa za kuwa bonde hilo linalalamikiwa na wananchi kuwa wanadhurumiwa mashamba yao Hamoud amesema kuwa hana taarifa zozote zilizomfikia ofisini kwake kuhusu mgogoro huo.

“Mimi ndio kwanza nasikia kwako kuwa bonde la Kiwalani linautata kwa wananchi na ninashangazwa na hilo kwa sababu kwenye mikutano yangu huwa nawauliza wananchi kama kuna matatizo yanayowakabili hawalisemi hilo,” amesema Hamoud.

Hamoud amesema kuwa mara kadhaa halmashauri imejaribu kuwasimamisha wakulima kufanya shughuli zao za kilimo katika bonde hilo lakini wamekuwa wagumu kukubali, hali iliyopelekea halmashauri kufungua kesi. Bado kesi hiyo haijatolea maamuzi.

error: Content is protected !!