Friday , 1 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Julius Mtatiro ‘avibwatukia’ vyama vya upinzani
Habari za SiasaTangulizi

Julius Mtatiro ‘avibwatukia’ vyama vya upinzani

Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF
Spread the love

WADAU mbalimbali wa masuala ya siasa za Tanzania wamezidi kutoa maoni yao kuhusu uchaguzi mdogo wa marudio ya udiwani ambao ulifanyika jana katika kata mbalimbali Tanzania Bara, anaandika Angel Willium.

Miongoni mwa wadau waliotoa maoni yao ni pamoja na mwanasiasa, Julius Mtatizo ambaye ni mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF).

Mtatiro ambaye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania bara na mgombea ubunge jimbo la Segerea mwaka juzi amesema licha ya kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinatumia nguvu nyingi kuwadhulum wapinzani, lakini pia kambi ya upinzani imeshindwa kuonyesha umoja na mshikamano.

Ametoa mfano kuwa katika Kata ya Lukumbule wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma, CCM kilipata kura 1572, CUF kura 1351, Chadema kura 234 na ACT kura 112 na kwamba kama vyama hivi vya upinzani vingeungana mgombea wao angeshinda.

Amesema hiki ni kielelezo kuwa vyama vyetu vinapaswa kujipanga na kwamba mwaka 2015 vilikosa majimbo muhimu karibia 20 kwa sababu hizi.

Uchaguzi wa marudio wa madiwani mwaka 2016, vilipoteza kata muhimu kwa sababu ya kuwekeana wagombea na kusababisha CCM ishinde kirahisi.

Mwaka huu 2017 kwenye kata zote upinzani haukuwa na maelewano na kwa hiyo vyama vilisimamisha wagombea bila kujali athari zake.

Wakati kukiwa na watu wanaoamini kuwa kuitoa CCM kunahitaji nguvu ya chama kimoja kimoja cha upinzani, mimi naamini kuwa CCM itapunguzwa nguvu ikiwa vyama vya upinzani vitashirikiana na kuachiana.

Pamoja na ubabe wa CCM kutumia nguvu za dola, bado upinzani unaweza kushinda kirahisi kwa kuunganisha nguvu.

Wapo watu watakuja na hoja za “chama changu”, “chama chetu” n.k. Mimi si muumini wa chama changu, ni muumini wa chama changu kushirikiana na vyama vingine kuleta mabadiliko.

Nina maana kuwa si lazima tushinde dola mwaka huu, ushirikiano unatuwezesha kupata ushindi zaidi na kupunguza nguvu za CCM.

“Kiburi chetu kikiendelea namna hii, mwaka 2019 CCM itatushinda vibaya. Silaha za CCM ni mbili tu ambazo ni maguvu ya vyombo vya dola na mgawanyiko na kukosekana kwa uthabiti kwenye ushirikiano wa vyama vya upinzani.

Vyama vyetu vinaweza kushindana na kuishinda CCM ikiwa vitadhibiti njia hizo mbili na kwamba njia ya kwanza inadhibitika kwa maumivu.

Njia ya pili haina kazi, iko upande wetu na tunaweza kuidhibiti bila shida, tatizo linakuwa kwamba tumekataa kufanya hivyo kwa sababu za ki-ubinafsi na kiburi na tunaamua kujimaliza.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 mathalani, kwa sababu ya UKAWA Chama cha CUF kilipata wabunge 10 Tanzania bara (huko nyuma enzi za Lipumba ilikuwa mbunge 0 au 2).

Pamoja na mafanikio hayo CUF ilikosa majimbo takribani 7 kwa sababu ya kuwekeana wagombea, na CHADEMA ilikosa majimbo kadhaa kwa sababu hiyo hiyo.

Pamoja na kazi ya kila chama kujijenga kwa kujitegemea, suala la kuuchukulia uchaguzi kama jambo la maisha ya watu halikwepeki.

Kuwekeana wagombea kwenye uchaguzi ni kuumiza demokrasia na kufifisha matumaini ya wananchi kuunga mkono mabadiliko.

Nchi zote za Afrika ambako vyama vya upinzani viliviondoa vyama tawala madarakani, upinzani ulifanya hivyo kwa kuungana.

Tanzania haitaweza kuleta mabadiliko ikiwa vyama vya upinzani havitatathmini upya ufanyaji siasa wake, kwenye chaguzi.

Navikumbusha vyama vyetu vya upinzani (hasa CUF, CHADEMA, NCCR na ACT) vifikirie haraka kujipanga kistratejia na kuachiana maeneo kwa dhati kwenye chaguzi zijazo.

Ni wazi kuwa kwa nguvu inayotumia na CCM hivi sasa, kunusurika kwa upinzani ni kuunganisha nguvu na watu wote wajue hivyo.

Kutounganisha nguvu (kwa maana ya nyakati za uchaguzi) kuna maana ya kushindwa kwa vyama vyetu kuwaletea wananchi matarajio na matamanio yao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mwili wa Hayati Mwinyi kuagwa leo saa 8 Uwanja wa Uhuru

Spread the loveMWILI wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi unatarajiwa kuagwa kuanza...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi kuzikwa Machi 2 visiwani Unguja

Spread the loveMWILI wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania,...

Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Mwinyi afariki dunia

Spread the loveRais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan...

Habari za Siasa

Waziri mkuu Ethiopia atua Tanzania

Spread the loveWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia,...

error: Content is protected !!