January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Julius Kalanga, mfalme mpya wa Monduli

Spread the love

Jimbo la Monduli, Arusha lenye historia ndefu ya kisiasa kufuatia kuwahi kuongozwa na mawaziri wakuu wastaafu wawili ambao ni hayati Moringe Sokoine na Edward Lowassa sasa lipo chini ya Julius Kalanga wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwa ndiyo nyota mpya inayong’ara katika jimbo hilo. Anaandika Charles William … (endelea.)

Julius Kalanga akipeperusha bendera ya Chadema katika jimbo la Monduli aliibuka na ushindi wa kura 35,024 huku akimuangusha mpinzani wake Namelock Sokoine wa Chama cha mapinduzi(CCM) aliyepata kura 25,925 na hivyo kuandika ukurasa mpya wa siasa za jimbo hilo.

Kwa upande wa madiwani, Chadema ilishinda kata madiwani 13 dhidi ya CCM iliyoambulia kata 7 jambo linaloashiria kuwa Chadema itaongoza halmashauri ya Monduli kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Mwanahalisi Online imezungumza na Julius Kalanga ambaye ni mbunge mpya wa jimbo hilo kuhusiana na kampeni zilizomalizika huku pia akielezea vipaumbele vyake kwa wananchi wa Monduli baada ya ushindi.

“Tatizo kubwa la kuanza nalo kwa sasa ni maji, tuna vyanzo kutoka Ngaramtoni kuja Monduli lakini kuna baadhi ya vijiji, maji bado hayajafika kwahiyo mimi nitaanza na suala hili kama kipaumbele changu cha kwanza”. Ameeleza Kalanga.

Wakati kampeni zikiendelea jimbo la Monduli, ilielezwa kuwa Kalanga angekumbana na upinzani mkali dhidi ya Namelock Sokoine wa CCM ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mwenye heshima kubwa Tanzania, Edward Moringe Sokoine.

Hata hivyo Julius Kalanga anasema kuwa ‘mzimu’ wa Sokoine haukuibuka wala kumsumbua kabisa katika uchaguzi huo isipokuwa alisumbuliwa na nguvu kubwa ya kifedha ya mgombea huyo pamoja na chama chake CCM.

“jina la marehemu Sokoine lilikuwepo hata kabla ya uchaguzi, umaarufu wake ulitokana na kazi alizozifanya na sio maneno kwa hiyo kama Namelock alikuwa mbunge viti maalum na hakuwatumikia wananchi hakukua na namna ambayo jina la baba yake lingembeba”. Anaeleza Kalanga.

Julius Kalanga ambaye aliwahi kuwa diwani kupitia CCM, kabla ya kuhamia Chadema anaeleza kuwa halmashauri ya wilaya ya Monduli chini ya Chadema itafanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ili kukata kiu ya mabadiliko kwa wananchi wa jimbo hilo.

“Kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, wananchi wa Monduli wameonyesha kiu ya kutaka mabadiliko na hatutaki kuwakatisha tamaa tunataka wasijutie kuiondoa CCM, tutafanya kazi kwa bidii” amesisitiza Kalanga.

Edward Sokoine, waziri mkuu katika serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere na Edward Lowassa ambaye pia alikuwa waziri mkuu katika serikali ya awamu ya nne wote wamekuwa wabunge katika jimbo la Monduli huku wakijizolea sifa nyingi, sasa ni zamu ya Julius Kalanga, ataweza kuwa mfalme mpya Monduli?

error: Content is protected !!