June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jukwaa la Wahariri walaani kuzomewa Mengi

Spread the love

JUKWAA la Wahariri (TEF), limelaani kitendo cha kuzomewa na kudhalilishwa kwa waandishi wa habari wa ITV, katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Dar es Salaam, Oktoba 30 mwaka huu. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Akizungunza na waandishi wa habari Katibu wa Jukwaa hilo, Neville Meena amesema kuwa kitendo hicho si cha kukaliwa kimya kutokana na kukwaza utendaji wa kazi na kudhalilisha utu wa waandishi hao mbele ya jamii.

Meena amesema kuwa waandishi na wafanyakazi wa kituo hicho walikuwa katika ofisi hizo za CCM, wakirusha na kuandika habari za tukio la mapokezi ya Dk. John Magufuli baada ya kukabidhiwa hati ya ushindi wa urais na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika hafla iliyofanyika siku hiyo katika ukumbi wa Diamond Jublee.

“Kuzomewa kwa waandishi hao katika ofisi za CCM ni muendelezo wa kile kilichoanzia Diamond Jubilee ambapo wafuasi wa Chama cha Mapinduzi CCM, walionekana wakiwazomea wafanyakazi wa ITV na baadaye kumzonga Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk Reginald Mengi ambaye ni mmliki wa kituo hicho,” amesema Meena.

Ametoa onyo kwa kuwataka wafuasi hao waache vitendo hivyo, akisema kuwa utafiti mdogo waliofanywa na Jukwaa hilo kuhusu vitendo hivyo vinatokana na wafuasi hao kuchukizwa na jinsi kituo hicho kilivyoripoti, matukio ya kampeni na kuwapa fulsa wagombea wa vyama vingine vya siasa.

Amesema kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vyombo vya habari vilivyofanya kazi zake kwa weredi wakati wa kampeni za wagombea wa vyama vyote nchi nzima ambapo Dk. Magufuli na Mgombea Mwenza, Samia Suluhu walikuwa na wandishi wa kituo hicho miongoni mwao ni Emmanuel Buhohera na Halfan Liundi ambapo umma wa watanzania ulipata kufahamu kinachoendelea katika mikutano yao ya kampeni.

Meena ameongeza kuwa hilo sio tukio la kwanza kufanywa na chama hicho kwani wakati wa kampeni za mgombea urais kilimfukuza katika msafara wa Dk. Magufuli mkoani Mbeya, mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias kwa madai ya kutofurahishwa na habari aliyoandika kuhusu mgombea wao.

Amesema kuwa matuko hayo siyo kiungwana na hayatakubalika katika jamii ya watu wastaarabu. Ikiwa waandishi wa habari au vyombo vya habari vinafanya makosa zipo njia za kisheria za kushughulikia makosa hayo pamoja na kufanya mazungumzo kupitia taasisi za waandishi wa habari.

“Tunachukua fulsa hii kuvitaka vyama vya siasa kama taasisi viongozi, wanachama na wapenzi wake kuacha mara moja vitendo vya kuwashambulia waandishi wa habari kwa sababu zozote zile. Tusingependa ifike hatua kutangaza kwamba matukio ya chama fulani ni hatari kwa waandishi wa habari,” amesema Meena.

Kadhalika tunachukua fursa hii kuvitaka vyama vya siasa na watu binafsi wanaoandaa mikutano inayowahusisha waandishi wa habari kuhakikisha kuwa waandishi wanakuwa salama wanapo hudhuria kwenye mikutano yao na kuchukua hatua ya kukemea.

“Tunasikitika kwa ukimya wa chama hicho ulionyesha kufurahishwa kwa tukio hilo kutokana na kutotoa kauli yoyote,” amesema Meena.

Matukio hayo yanajirudia kwa waandishi ikiwa pamoja na lile la mwandishi wa Uhuru kupigwa Chadema, chama cha ACT-Wazalendo kuwagomba baadhi ya waandishi wa habari na vyama vengine vya siasa ikiwa wanawatumia waandishi hao katika kufikisha sera zao licha ya kuwepo kwa vikwazo kwa Jeshi la polisi na baadhi ya watumishi katika ofisi mbalimbali ambao kwa namna moja au nyengine wanakandamiza uhuru wa habari.

error: Content is protected !!