Thursday , 18 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kina Kibamba waishika pabaya Serikali
Habari za SiasaTangulizi

Kina Kibamba waishika pabaya Serikali

Deus Kibamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (kulia) anayefuata ni Hebron Mwakagenda, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukata. Picha ndogo Rais John Magufuli
Spread the love

KUPITIA bajeti  ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa miaka miwili mfululizo (2016/2017 na 2017/2018) serikali ilitazamiwa kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa mchakato wa katiba mpya, anaandika Pendo  Omary.

Lakini mpaka sasa hakuna maelezo ya kina juu ya hatma ya mchakato huo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Hebron Mwakagenda, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) anasema kwa kuwa hakuna bajeti yoyote iliyotenngwa kwa ajili ya kazi hiyo ni ngumu kupatikana katiba mpya kwa sasa.

“Kwa mazingira yaliyopo, kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kumebaki fursa  finyu ya kuandaa bajeti ya dharura na kuipitisha katika kipindi hiki cha mwaka  2017,” anasema Mwakagenda.

Maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa yanatakiwa yawe yameanza rasmi muda mfupi kuanzia sasa na uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2019.

Aidha, uchaguzi mkuu ujao ambao utafanyika mwezi  Oktoba 20120 unapaswa kuwa umeanzishwa maandalizi yake kuanzia mwakani,  2018 ukiwemo uandikishaji na uhakiki wa wapiga kura yanapaswa kuwa yameanza ifikapo mwezi Januari 2018.

Anaeleza kuwa kwa sasa yapo matukio mengi ya kikatili yanayoendelea nchini ambapo kama Katiba mpya iliyopendekezwa na wananchi ingekuwa imekamilika ingesaidia kuyapunguza au kuyamaliza kabisa.

Anayataja matukio hayo kuwa ni; kuzuiwa kuoneshwa Bunge moja kwa moja kwenye Luninga (mubashara),  polisi kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa vya upinzani,  polisi kukamata wabunge, viongozi na viongozi waliopo nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kutungwa kwa sheria zinazozuia uhuru wa wananchi kujieleza, kutishiwa, kutekwa, kupotezwa, kuumizwa na kuuawa kwa wabunge, viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani na wananchi wengine, matumizi mabaya ya mamlaka ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, CCM  kuendelea na mikutano na shughuli mbalimbali za kisiasa bila kubugudhiwa na polisi ni matukio yanayoweza kudhibitiwa na katiba mpya ya wananchi,” anasisitiza Mwakagenda.

Anatolea mfano wa tikio la kupigwa risasi Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrsaia na Maendeleo (Chadema), Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mbunge wa Singida Mashariki na mwaharakati nguli kuwa ni  ukiukwaji wa katiba.

“Ni fedheha kwa taifa linalojulikana kama kisiwa cha amani na utulivu kwa kitendo cha kumshambulia mtu asiye na hatia kwa risasi zaidi ya 30. Jukata tumesikitishwa na kushangazwa na uonevu  na ukatili aliofanyiwa Mh. Lissu,” anaeleza Mwakagenda

Mwakagenda anasema kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Kenya tarehe 8 Agosti, mwaka huu na hatimaye kufutwa na Mahakama ya juu ya Kenya tarehe 1 Septemba, hatua hiyo inaonesha uimara wa Katiba ya Kenya iliyopitishwa rasmi mwaka 2010.

“Ni funzo kwa Tanzania kufuatia uchaguzi wa Kenya wa mwaka huu ni kwamba kuna umuhimu na ni wakati muafaka sasa kwa matokeo ya Rais atakayechaguliwa na Watanzania kuhojiwa mahakamani,” anaeleza Mwakagenda.

Aidha, Mwakagenda anasema kama ikitokea hakuna uwezekano wa kukamilisha mchakato wa katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama ambavyo dalili zinavyoonyesha kunahitajika marekebisho ya msingi (Minimum Reforms).

Marekebisho hayo lazima yahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na vifungu vya Sheria zote zinazohusu uchaguzi ili kushughulikia kasoro zote zinazolalamikiwa kwenye uchaguzi wa Tanzania.

Anayataja maeneo yanayohitaji mapendekezo ya marekebisho kuwa ni yale yanayohusu: uhuru wa Tume ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, fursa ya mgombea huru katika uchaguzi wa Tanzania, uwezekano wa kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais Mahakamani na kuwezesha vyama vya siasa kuungan kikatiba na kisheria kwa lengo la kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi .

Marekebisho mengine yanahusu kurejesha mfumo wa ushindi katika uchaguzi wa Rais kwa kigezo cha kupatikana kwa kura zisizopungua asilimia 51 ili kuhakikisha kuwa mgombea urais anayeshinda anakuwa na ridhaa ya Watanzania walio wengi.

“Pia ni muhimu kuingiza katika katiba na kwenye sheria za uchaguzi uwakilishi sawia kati ya wanawake na wanaume katika vyombo vya maamuzi kama vile mabaraza ya madiwani, Bunge, Baraza la Wawakilishi ili kuakisi dhana na nia iliyomo katika mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na serikali,” anaeleza Mwakagaenda.

Amasema kwa sasa Jukata imejikita katika awamu ya program kubwa ya kutoa elimu ya uraia ikihusisha mchakato wa katiba mpya ulipofikia, mambo yanayopaswa kufanywa wakati wa mpito kuelekea ukamilisjhwaji wa mchakato pamoja na masuala ya kimaudhui.

“Itakuwa ni heshima kubwa kwa serikali ya awamu ya tano kama itawezesha ukamilishwaji wa katiba mpya ya wananchi katika kipindi hiki kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Vinginevyo, itabaki katika histoaria kwamba serikali ya wamu ya tano ilizima ndoto za Watanzania kupata katiba mpya iliyokuwa imejengeka katika fikra zao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!