April 12, 2021

Uhuru hauna Mipaka

JPM atoa onyo kwa wafanyabiashara

Spread the love

RAIS John Magufuli amewataka wafanyabiashara kujenga tabia ya kuwa wakweli kwani, wanapokuwa waongo husababisha serikali kuchukua uamuzi ambao pengine huonekana kutokuwa rafiki kwao. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza kwenye kikao cha pamoja na wafanyabiashara hao Ikulu, jijini Dar es Salaam leo tarehe 7 Juni 2019, alitaja baadhi ya kampuni ambazo zimekuwa zikidanganya faida ambazo imekuwa ikizipata ili kupunguza kodi.

Akitaja kwa majina baadhi ya kampuni hizo amesema, zimekuwa zikipeleka taarifa ya uongo Mamlaka ya Mapato (TRA) kinyume na taarifa ya mapato inayooneshwa kwenye taarifa ya fedha za benki (Bank Statement).

“Mnapaswa kuwa wakweli, wakati mwingine mnasababisha serikali kuchukua uamuzi pengine sio ratifiki,” amesema Rais Magufuli akisisitiza kuwa, wafanyabiashara waache kutoa taarifa za uongo pale wanapotakiwa kulipa kodi.

Ametoa mfano kuwa, kampuni moja ilipata faida zaidi ya Sh. 500 milioni kwa mujibu wa taarifa ya fedha ya kibenki (Bank Statement), lakini taarifa ya TRA ilionesha imepata faida Sh. 73 milioni.

Kwenye kikao hicho na wafanyabiashara hao kutoka nchini kote amesema, kikao hicho kinalenga kusaidia kuboresha mazingira ya kibiashara kwa wafanyabiashara kwa kueleza changamoto wanazokumbana nazo na namna ya kuzitatua.

Rais Magufuli ambaye alianza kuongoza taifa hili tarehe 5 Novemba 2015, amewaalika viongozi wengine wakuu kutokana na umuhimu wa kikao hicho, miongoni mwa walioalikwa ni Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais; Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu na mawaziri wengine.

Amesema kuwa, sekta hiyo ya biashara ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi na kwamba, serikali itaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuimarisga mazingira ya biashara nchini ikiwa ni pamoja na kusimamia amani.

“Palipo na amani ndipo biashara hufanyika vizuri, kinyume chake panapokosekana amani, kila kitu kinakuwa tofauti,” amesema.

 Hata hivyo amesema, amefuta tozo 101 kwenye kilimo, uchimbaji madini, uvuvi, ufugaji, lengo likiwa ni kuendelea kuboresha mazingira ya kazi hizo.

“Kodi zikiwa chache na viwango vikiwa vidogo, biashara inastawi, kinyume chake kodi ikiwa kubwa, biashara zinadumaa na hii ndiyo sababu tumeanza kuchukua hatua,” amesema.

error: Content is protected !!