April 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

JPM arejesha matumaini wakulima wa korosho

Zao la Korosho

Spread the love

RAIS John Magufuli amerejesha matumaini kwa wakulima wa zao la kibiashara la korosho ambao bado hawajalipwa fedha zao mpaka sasa. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Ameagiza mamlaka husika kutoa kiasi cha Sh. 50 bilioni ili kuendelea kulipa wakulima 18,000 waliofanyiwa uhakiki haraka.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 2 Aprili 2019, wakati akihutubia katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara.

Pia ameagiza kuwa, wakulima wenye wastani wa kilo zaidi ya 1,500 kila mmoja na kuendelea, kuanza kulipwa fedha zao kuanzia kesho tarehe 3 Aprili 2019.

“Hawa walikuwa 18,103, ndio wamepatikana hao hawajalipwa, wenye kilo nyingi zaidi ya 1,500 waliolipwa wachache.  Sasa uchambuzi umekamilika tusingezweza kulipa bila uchambuzi.

“Nimeishatoa maagizo ziletwe bilioni 50 kuanzia kesho na kesho kutwa hawa nao waanze kulipwa, na zikiisha tunaleta zingine,” amesema.

Aidha, Rais Magufuli ameagiza wale walionunua korosho kabla ya kuvunwa ‘Kangomba’ kuzipeleka kwa ajili ya kulipwa fedha zao, huku akiwaagiza kuleta vithibitisho vya kisheria vinavyothibitisha ununuzi wa korosho hizo.

“Lakini katika hili nataka niliweke wazi, najua wako walikuwa wananunua korosho ziko mashambani, wengine wamenunua maua kwamba yakichanua ni yangu, ninafahamu imekuwa biashara iliyozoelekea lakini sio nzuri sababu imekuwa inadhulumu wananchi.

“Kukiri ni jambo zuri, wale waliokiri walikuwa ni kangomba, wanaomba serikali iwasamehe iwalipe, ninasema muwaangalie na hao muwalipe, najua waliofanya hivyo ni wengi hata mwenyekiti wangu wa CCM wa mkoa alikuwa anahangaika, ninafahamu kufanya kosa si kosa lakini kurudia ni kosa,” amesema Rais Magufuli.

Pia ameonya watu wanaojihusisha na biashara ya Kangomba, akiwataka kutorudia tena “mwaka huu tumewapa taarifa, tafadhalini jamani msiwaumize wakulima wadogo, wananchi wanakuwa watumwa kwa mazao yao, sasa upigwe na kangomba wakija ushirika wanapiga kangomba yake.”

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema hadi sasa serikali imekwishatoa kiasi cha Sh. 578.7 bilioni kwa baadhi ya wakulima wa korosho.

“Serikali iko pamoja na ninyi, na ndio maana mpaka hapa ninapozungumza, fedha ambazo zimelipwa ni bilioni 578.7 kwa wakulima wa korosho,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!