August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JPM angejua, asingethubutu

Spread the love

KWA kauli na mwenendo wa utawala wake, Rais John Magufuli hapendi upinzani. Hapendi kukosolewa. Anafanya jitihada zote anazoweza kuhakikisha yeye pekee ndiye anabaki katika majukwaa ya siasa. Anawaambia wanasiasa wengine wasubiri hadi 2020, anaandika Rwazi Rwakatanga.

 Hata kwa kutazama na kutafakari hatua za jeshi la polisi dhidi ya vyama vya upinzani, ni rahisi kujua kwamba wanafanya hivyo ili kutii amri na kufurahisha wakubwa wanaowatuma, lakini nao wanajua kuwa wanavunja sheria.

Serikali ya Magufuli inajaribu kufanya kile ambacho kilishindikana miaka 25 iliyopita, kilichoshinda wana CCM walioiambia Tume ya Jaji Nyalali kwamba, hawako tayari kukaribisha mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Upenyo pekee walionao watawala ni sheria mbovu zilizoorodheshwa miongoni mwa zile 40 ambazo Tume ya Jaji Nyalali ilishauri zirekebishwe au zifutwe, na zilizoongezeka baadaye, kwa kuwa haziendani na dhana ya demokrasia katika mfumo wa vyama vingi.

Zipo nyingi, lakini zinazotumiwa zaidi kuumiza wananchi ni Sheria ya magazeti, sheria ya magereza, sheria ya usalama wa taifa, na sheria ya makosa ya mtandaoni.

Ni sheria kandamizi, za kikatili, zinazominya uhuru wa watu kufikiri, kujumuika, kuwasiliana, kubadilishana mawazo na kupeana taarifa.

Jambo moja ambalo Magufuli na serikali yake wameshindwa kung’amua ni kwamba kadiri wapinzani na wakosoaji wa serikali wanavyoteswa, ndivyo wanavyoimarika.

Miaka 25 ya mateso ya wapinzani haikufaulu kuzima vuguvugu la mabadiliko. Bunge lililokuwa na mbunge mmoja wa upinzani mwaka 1993, sasa lina wabunge zaidi ya 100 wa upinzani. Kuna maelfu ya kata, vijiji, vitongoji, na mitaa vinavyoongozwa na wapinzani.

Kwa tathmini yoyote ile, upinzani umekuwa unaogezeka nguvu, si kwa hiyari ya watawala, bali kwa matakwa ya wakati. Kwa hiyo, kama serikali ya awamu ya tano isubiri kushangazwa na takwimu miaka minne ijayo.

Rais Magufuli anaogopa maoni tofauti, na anafikiri kwamba njia sahihi ya kuhakikisha anabaki peke yake ni kuzuia wengine kufanya siasa.

Anajua kuwa amri anazotoa hazitekelezeki. Anafahamu kuwa zinagongana na katiba ya nchi, inayotambua vyama vya siasa. Anajua kuwa zinakinzana na sheria ya vyama vya siasa (1992), inayosimamia shughuli za wanasiasa na wafuasi wao.

Lakini hajajua mambo matatu; kwamba kadiri anavyotumia polisi kuzima upinzani kwa nguvu zote, tunakoelekea, yeye na polisi wanaweza kuiingiza nchi hii katika mzozo mkubwa ambao unaweza kumwingiza kwenye matata yaliyokumba viongozi wengine wababe kabla yake.

Pili, asilojua ni kwamba hata kama hataki wapinzani wazungumze, watazungumza, kwani hatafanikiwa kurudisha nchi miaka 25 nyuma.

Tatu, asilotambua ni kwamba uimara wa nchi utatokana na uhai wa upinzani, siyo vigelegele vya makada wa CCM. Kwa kuzuia upinzani, rais anapanda mbegu ya uozo wa serikali yake na anaweka mbolea kwenye kitalu cha upinzani.

 

error: Content is protected !!