May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JPM amwangukia Maalim Seif

Spread the love

DAKTARI John Magufuli, Rais wa Tanzania amemwomba Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kumsaidia Dk. Hussein Ali Mwinyi, rais wa visiwa hivyo ‘kuinyoosha’ nchi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).

Amemtaka Rais Mwinyi kutoogopa kutumbua majibu kwa maslahi ya Zanzibar, na kwamba kwa mwendo waliouanza viongozi hao wawili, anatumai Zanzibar itakuwa kama Dubai.

“Usiogope kutumbua majipu, wanaokwamisha watumbue. Maalim Seif msaidie sana mheshimiwa rais katika kuhakikisha masuala ya mali za umma, mali za wanyonge zinasimamiwa kikamilifu,” amesema Rais Magufuli wakati akizungumza mbele ya viongozi hao waliokuwa kwenye zaira Chato, Geita.

Rais Magufuli amesifu maafikiano yaliyofikiwa kati ya Maalim Seif ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo na Dk. Mwinyi, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

“Maalim Seif uliacha interest (manufaa) zako, ukafuata interest za nchi yao, wewe ni kiongozi kweli. Nilifahamu Zanzibar ya Hussein Mwinyi itakuwa ya tofauti.

“(Hussein Mwinyi) ni jasiri, mnyeyekevu ana heshima na mchapakazi. Nampongeza Mwinyi kwa hatua za mwanzo katika utawala wake, mapato yanaanza kuongezeka, ufisadi unapungua kila senti itakayokusanywa, itatumika Zanzibar,” amesema Rais Magufuli na kuongeza:

“Nampongeza pia Maalim Seif kwa sababu katika umoja wao, tumeanza kuuona mwanga wa maendeleo Zanzibar. Ndio maana Rais Mwinyi alivyotaka kuja kuniona na Maamlim Seif, sikukataa kwasababu nimeanza kuona maendeleo ya Zanzibar.”

Rais Magufuli amewaeleza Maalim Seif na Dk. Mwinyi kwamba, atakuwa nao karibu katika hatua zao za maendeleo na “mimi kama Rais wa Tanzania, nawahakikishia sapoti kwa maendeleo ya Wazanzibari. Sitawacha kamwe.”

Amesema, Maalim Seif na Rais Mwinyi, wote kwa pamoja wanahubiri amani, huku akikumbusha kwamba zipo ndoa zilizoparaganyika kutokana na tofauti za kisiasa lakini sasa zimeunganika.

“Zipo ndoa zilizovunjika kwasababu mwanamke alipigia CCM mwanaume ADC… nini vile, ACT (ACT-Wazalendo), siku ile waliungana.

“Maalim Seif ukitaka kuoa CCM hapa Chato ruksa, tunatakiwa tutangulize maslahi ya nchi yetu kwanza. Maadui zetu wangefurahi sana kuona tunagombana,” amesema Rais Magufuli.

Amesema, Rais Mwinyi anatoka Unguja, makamu wake wa kwanza (Maalim Seif) anatoka Pemba na makamu wake wa pili anatoka Pemba pia.

“Kwa hiyo, katika viongozi wakuu watatu wa serikali ya Zanzibar, wawili wanatoka Pemba. Hii ina maana kubwa katika uongozi, Mheshimiwa Hussein Mwinyi nakupongeza kwa hilo, umejenga upendo mkubwa,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!