RAIS John Magufuli amepuuza tuhuma zilizotolewa na Janeth Mbene, Mbunge wa Ileje kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya Haji Mnasi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, kwamba hana ushirikiano. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Licha ya Mbene kumchongea Haji kwa rais leo tarehe 5 Oktoba 2019, kiongozi huyo wa nchini amesema ‘simfukuzi’.
Mbunge huyo alimwambia Rais Magufuli, kwamba mteule wake (Haji) hana ushirikiano na watendaji wengine katika halmashauri hiyo, hivyo kusababisha utendaji kuwa mgumu.
Akizungumza na wananchi kwenye mji mdogo wa Mpemba, mkoani humo, Rais Magufuli amesema, hana taarifa za tuhuma anazohusishwa Haji ikiwemo wizi.
“Sasa mkurugenzi simtoi hadi nipate taarifa zangu mwenyewe,” amesema Rais Magufuli na kuongeza; “…sina uhakika kama dhambi zote hizo ni za mkurugenzi.
“Taarifa niliyonayo mimi na Jafo (Seleman-Waziri wa Tamisemi ni shahidi kwamba huyu mkurugenzi saa nyingine anaacha kazi zake za ofisini anaenda kufundisha darasani.”
Akizungumzia tuhuma za Haji, Rais Magufuli amesema hawezi kuchukua hatua yoyote jambo ambalo litakuwa uonevu.
“…mkurugenzi uko hapa, sikutoi mpaka nipate information (taarifa) zangu mwenyewe,” kauli hiyo ilipokelewa kwa tabasamu na mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, kwenye mkutano huo alikuwepo Suleiman Jafo, Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambapo rais alimuuliza kuhusu tuhuma anazobebeshwa Haji.
Jafo alimjibu Rais Magufuli kwamba katibu wa wizara hiyo yupo kwenye uchunguzi. Mdipo Rais Magufuli aliposema “mnaona, kumbe hata hiyo taarifa haijafika kwa Waziri wa Tamisemi, sasa mimi nichukue hatua tu yakufukuza mtu? ati jamani si nitawaonea watu kila mahali?.”
Leave a comment