MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania kutomchagua mgombea anayehubiri Serikali za Majimbo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tabora … (endelea).
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za CCM wilayani Urambo, Tabora leo tarehe 21 Septemba 2020, Dk. Magufuli amesema, utawala wa majimbo haufai kwa kuwa, ni chanzo cha mifarakano na ubaguzi.
“Ukitengeneza majimbo ya utawala katika nchi, huo ndio mwanzo wa mfarakano sababu kila jimbo unajitgemea mwenyewe, ukiwa masikini unakuwa masikini.
“Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa anaomba Uhuru wa Taifa hili, angeligawa katika majimbo, tusingefika hapa. Tuna makabila mengi Nyerere alituweka kama Taifa moja,” amesema Dk. Magufuli.
Hivi karibuni, Tundu Lissu, mgombea wa urais wa Tanzania kupitia Chadema katika kampeni zake wilayani Mufindi, Iringa aliahidi kuunda serikali za majimbo endapo atachaguliwa kuongoza taifa hili.

Kwenye mkutano huo, Lissu alisema anataka kila mahali wanufaike na rasilimali zilizoko katika maeneo yao. Hata hivyo, hiyo ni sera ya cham a hicho kikuu cha upinzani nchini.
Akisisitiza ‘ubaya’ wa Serikali za Majimbo, Dk. Magufuli ameeleza “ndio maana Tanzania katika miaka yote hatukuingia mifarakano kati ya makabili na makabila, kati ya maeneo na maeneo, sitaki kutoa mifano ya nchi ilizoingia katika mtego wa majimbo, hayo ndio mambo wanayofundishwa wanakotoka na lengo ni kuvuruga nchi ili watu wawe wanasomba mali.”
Amewataka wananchi kutokubali uongozi wa majaribio kwa kutengeneza serikali za majimbo, kwa kuwa itarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Tusikubali kuwekwa kwenye majaribio ya kutengenezewa majimbo, nchi hii imepiga hatua kubwa kubwa hatuwezi rudishwa nyuma,” amesema Dk. Magufuli.
Leave a comment