February 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

JPM ambana mbunge wa Chadema, atamani kuhamia CCM

Spread the love

MBUNGE wa Serengeti kupitia Chadema, Marwa Lyoba amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wafuasi wa CCM alipobanwa na Rais John Magufuli kuhusu matumizi ya kiasi cha Sh. 58 milioni, fedha  zinazotolewa na bunge kila mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya majimbo. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Tukio hilo limetokea leo tarehe 6 Septemba, 2018 katika mkutano wa hadhara wa Rais Maguguli na wakazi wa jimbo hilo.

Alipoulizwa na Rais Magufuli juu ya matumizi ya fedha hizo katika kutatua kero za wananchi, Lyoba alijikuta akiwahoji wafuasi hao wa CCM kwamba wanamzomea kwa sababu ya utofauti wa chama, huku akisema kuwa hata yeye anaweza kuwa CCM.

 “Sasa mnanizomea kwa sababu nyie ni CCM, hata mimi ninaweza kuwa ni CCM,” amesema Lyoba baada ya kukumbwa na kadhia ya kuzomewa na WanaCCM.

Katika maelezo yake, Lyoba alisema kuwa fedha hizo hutoa kwa kugawa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kijamii, ambapo asilimia 90 ya vijiji vilivyomo kwenye jimbo la Serengeti vimepata sehemu ya fedha hizo.

Rais Magufuli alichukua hatua ya kumhoji Lyoba kuhusu matumizi ya fedha hizo, baada ya mbunge huyo wa Chadema awali kumchongea Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamis kwamba amefanya ufisadi wa kiasi cha Sh. 20 milioni fedha zilizotoka Serikali kuu.

Akihoji kuhusu matumizi ya fedha anazopewa Mbunge Lyoba kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya jimbo, Dk. Magufuli alisema kuwa, alipokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Nata kuwa mbunge huyo hajawahi kupeleka fedha kwenye shule hiyo, na kwamba yeye Rais alitoa Sh. 5 miliini kwa ajili ya kusaidia shule hiyo.

“Na wanafunzi wa Nata walilalamika hawana kitanda, nikauliza mmepata kiasi gani kutoka kwa mbunge wakasema hawajapata nikachangia Sh. 5 milioni pale,” amesema.

Naye Hamis aliyetuhumiwa kula Sh. 20 milioni, katika utetezi wake, alisema kuwa fedha hizo ziliombwa na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) kwa ajili ya kusaidia shughuli za kijamii, ambapo milioni 10 zilitolewa kwa ajili ya Mwenge na milioni 10 zilitolewa kwa ajili ya kusaidia Shule ikiwemo shule ya  Sekondari ya Mara Day.

“Mikono yangu ni safi na salama, wilaya hii ni changam sijaiba hata senti tano. Hiyo fedha imeombwa na ofisi ya ras kama mchango, Milioni 10 ilienda Mara Day, na milioni 10 kwa ajili ya Mwenge. Mkoa wa Mara na wilaya zetu ni za upinzani, binafsi nilikuwa sina ugonjwa wa moyo nimeupata kwa kuwatumikia watu wa Serengeti,” amesema.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli alimpongeza mkurugenzi huyo na kuahidi kuwa hatomfukuza kazi kutokana na kufurahishwa na utendaji kazi wake.

“Katika siasa za vyama vingi wako watu wanataka kumsahau Mungu. Mimi nafahamu wakurugenzi wangu ninaowateua huwa wana apa, mimi nimefika Nata nimeangalia jengo la hospitali nikalinganisha na shule ya msingi iliyoko kulia nimeona utofauti.

Nakupongeza mkurugenzi umejieleza vizuri na wala sikufukuzi utabaki hapa hapa. Nilifikiri mimi mkurugenzi mwizi kweli leo ningemfukuza, mtu anazungumza mwizi mwizi nikaagiza watu wamchunguze nikakuta hana hatia,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!