August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JPM afura, Wizara ya Afya wapagawa

Spread the love

TAARIFA zilizoripotiwa leo, katika vyombo vya habari mbalimbali kuhusu upungufu wa dawa hapa nchini, zimeitibua Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, anaandika Charles William.

Taarifa kutoka wizarani hapo zinaeleza kuwa, Rais John Magufuli, mapema asubuhi ya leo baada ya kusoma taarifa za upungufu wa dawa, amehoji usahihi wa taarifa hizo na kutaka maelezo rasmi kuhusu dawa zilizopo nchini kama zinakidhi mahitaji au la.

Mchana wa leo, makao makuu ya Wizara ya Afya, jijini Dar es Salaam, palionekana kuwa na hekaheka ambazo zimeendana na vikao vya watendaji wa wizara hiyo pamoja na maofisa wa juu wa Bohari Kuu ya Dawa hapa nchini (MSD).

Chanzo chetu cha taarifa kutoka eneo hilo kimesema, “Vikao vya MSD na wizara vinafanyika tangu asubuhi ya leo ili Waziri Ummy Mwalimu apewe taarifa rasmi, inayotakiwa kwenda kwa rais kwasababu anataka maelezo juu ya upungufu wa dawa uliopo.”

Licha ya wizara hiyo, kuviita vyombo vya habari saa sita kamili leo mchana ili kuzungumzia sakata hilo lakini waaandishi wa habari walilazimika kukaa ukumbini kwa zaidi ya saa moja na dakika 5 wakiwasubiri maofisa wa wizara hiyo.

“Kati ya aina za dawa muhimu 135 zinazohitajika, aina ya dawa 71 sawa na asilimia 53 ya dawa zinapatikana katika bohari yetu hapa nchini,” amesema Dk. Mpoki Ulisubisya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano.

Dk. Mpoki amekiri kuwa upungufu wa dawa upo kwa asilimia 47 kwa sasa, ikiwa ni karibu nusu ya mahitaji. Hata hivyo amedai kuwa, kabla ya mwaka huu kumalizika, upungufu wa dawa utakuwa umepungua mpaka kufikia asilimia 35.

Baada ya waandishi kuhoji juu ya baadhi ya maofisa wa hospitali mbalimbali hapa nchini kulalamikia upungufu mkubwa wa dawa, Dk. Mpoki amesema, “Sijaja hapa kubishana na waandishi wa habari, nimekuja kutoa hapa taarifa tulizonazo sisi.

MSD haipeleki dawa katika vituo vya afya kutokana na utashi wake, inapeleka dawa kila baada ya miezi mitatu kutokana na maombi ya vituo husika vya afya, waulizeni hao wakuu wa vituo vya afya kwanini hawana dawa?”

Kuhusu deni kubwa ambalo serikali inadaiwa na MSD kiasi cha kuathiri ufanisi wa bohari hiyo ya dawa, Dk. Mpoki amekiri kuwa deni hilo ni kikwazo katika ufanisi wa MSD hata hivyo amesema serikali imejipanga kulipa asilimia kubwa ya deni hilo.

“Tunadaiwa 132 bilioni lakini katika hotuba ya Bajeti iliyosomwa Bungeni na Waziri tuna mpango wa kuilipa MSD zaidi ya 251 bilioni kwahiyo tutakuwa tumepunguza deni hilo kwa kiasi kikubwa,” amesema.

error: Content is protected !!