March 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Josephine Mushumbusi atajwa kesi ya Lulu

Elizabeth Michael 'Lulu' (mwenye hauni jekundu) akiwa mahakamani. Picha ndogo Josephine Mushumbusi mmoja wa mashahidi wake

Spread the love

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemtaka askari aliyerekodi ushahidi wa Josephine Mushumbusi kufika mahakamani kutoa ushahidi kwenye kesi inayomkabili Elizabeth Michael (Lulu), anaandika Faki Sosi.

Mushumbusi ni mmoja wa mashahidi muhimu katika kesi ya msanii huyo ambaye alichukuliwa maelezo yake.

Lulu anatuhumiwa kumuua bila kukusudia msanii mwenzake aliyekuwa ana mahusiano naye kimapenzi, Steven Kanumba.

Leo katika mahakamani hiyo, wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliwasilisha ombi la kusoma maelezo ya shahidi ambaye hayupo nchini na kwamba hataweza kupatikana.

Wakili wa serikali, Faraja George amepinga ushahidi huo kwa madi kwamba wakili wa utetezi hana mamlaka wala hawezi kufanya kazi ya ushahidi.

Baada ya mabishano hayo, Jaji Sam Rumanyika amesema kuwa ushahidi huo utatolewa na askari aliyerekodi maelezo ya shahidi ambaye ni sajent Nyange mwenye namba E103.

Katika hali isiyo ya kawaida Lulu alitimua mbio mara baada ya kutoka mahakamani huku sauti za ndugu zake zikisikia zikisema ‘Lulu kimbia’. Mshtakiwa huyo alikimbia kuzikwepa kamera za wanahabari waliokuwepo mahakamani hapo.

Kesi hiyo ambayo imesikilizwa mfululizo kuanzia wiki iliyopita itaendelea kesho Octoba 25.

error: Content is protected !!