Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Joseph Selasini: Muongo au msahaulifu?
Makala & Uchambuzi

Joseph Selasini: Muongo au msahaulifu?

Joseph Selasini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi
Spread the love

 

ALIYEKUWA mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Rombo, mkoani Kilimanjaro, Joseph Selasini, ameibuka upya na kudai kuwapo mkakati unaosukwa na waliokuwa “marafiki zake,” mimi nikiwamo, kumchafua na kumvunjia hadhi yake mbele ya jamii. Anaandika Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Anasema, mgogoro wa uongozi unaofukuta ndani ya NCCR- Mageuzi, kwa kiasi kikubwa, unachochewa na hatua ya baadhi yetu, kutumiwa na mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.

Alisema, “…najua kabisa, najua ndiyo maana namuambia Mbatia, amwambie Kubenea aache, kwa sababu, mimi naweza kutoa ya familia yake, kwa kuwa tunafahamiana. Hata Kubenea, naweza kutoa ya kwake pia. Ninamfahamu. Sisi tumekuwa wote kwa muda mrefu.

“Lakini mimi ni mtu mzima, nakwenda kwa hoja. Mimi siendi kwa mambo ya Kiswahili. Yaani watu wanachukulia vitu kwa mambo ya mtaani, katika mambo mazito. Siyo sahihi kusema kuwa huyu hastahili katika jamii, kwa kuwa ni mhuni, ili nini? Sisi tunaangalia nini analeta, si uhusiano wake,” alieleza.

Msingi wa madai ya Selasini, ni taarifa zinazoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, zikimnukuu Dk. Masumbuko Lamwai, mmoja wa wanawazuoni mashuhuri nchini, akielezea maisha ya Selasini, mwenendo wake, tabia zake na hulka yake.

Dk. Lamwai, aliyekuwa mhadhiri mwandamizi wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mbunge wa Ubungo na Mkurugenzi wa Katiba na Sheria (NCCR-Mageuzi), ameeleza mengi kuhusu mwanasiasa huyu.

Aidha, Dk. Lamwai, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, diwani wa kwanza wa upinzani katika Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, kupitia kata ya Manzese na baadaye Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, na Joseph Roman Selasini Shao, ni watoto wa Mzee Roman Selasini na mkewe, Katharine Shao.

Kutokana na uzito wa kile kilichoelezwa na Selasini, nimelazimika kujibu baadhi ya madai yake, ili kuweka rekodi sahihi.

Kwanza, kauli ya Selasini ya kutaka umma upuuze maandishi ya Dk. Lamwai, siyo sahihi. Haiwezekani kuwa Dk. Lwamwai, alikuwa zuzu, na kwamba alifanya mambo ambayo hayajui na hayaamini.

Dk. Lamwai, ni mmoja wa wanazuoni nguli nchini, na kwamba hata aliyekuwa Rais wa Jamhuri, Benjamin Mkapa, aliwahi kukiri hilo hadharani.

Kwa maneno yake, Mkapa alisema, “Dk. Lamwai ni mtu mahiri mwenye uwezo wa kujenga hoja na kuibomoa.” Hivyo basi, hata maandishi yake, hayawezi kupuuzwa. Yataendelea kuishi.

Ningemuelewa Selasini katika utetezi wake, kama angeangalia maudhui ya maandishi ya Dk. Lamwai, badala ya kushambulia wanaofanya rejea.

Hii ni kwa sababu, yaliyorejewa hayakuandikwa na mimi. Yameandikwa na Lamwai mwenyewe, na kama mwenyewe angekuwapo leo, bila shaka angemjibu vilivyo.

Pili, Selasini aache kutisha watu. Kama yeye analo la kusema, kuhusu mimi basi aseme. Asinitishie na wala kufahamiana kwetu, hakuwezi kuwa kinga.

Ni muhimu akafahamu kuwa tofauti zetu, zimetokana na hatua yake ya kutaka kukabidhi chama cha watu, mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ugomvi wetu wa leo na hili asilikwepe, ni yeye kutaka kukidalalia chama cha watu.

Hakuna mwenye kufikiri vizuri, anayeweza kukubali kuwa unaoitwa, “mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC),” na ambao yeye aliutumia kutangaza kuwa Mbatia amesimamishwa uongozi, waweza kuwa halali, kwa vigezo vyovyote vile.

Ni mkutano uliofanyika kinyume na katiba ya chama hicho na ulikuwa na mikono ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Yaani wanaohubiri kutaka kuondoa CCM madarakani, ndio hao hao wanageuka mawakala wake.

Wala hakuna uhalali wa kuwa mwanzilishi wa mageuzi, kuwa na mamlaka ya kuyaua. Ndio maana hata mzazi anapotaka kumuua mtoto wake, jamii inachukua jukumu la kumdhibiti. Haimuachi kwa kuwa ni mtoto wake.

Tatu, nimemsikia Selasini akitamba kuwa suala la uhuni, siyo hoja. Kinachoangaliwa, unachozalisha. Huu ni upotoshaji mkubwa.

Mhuni hawezi kuwa kiongozi wa umma. Na kama anakiri yeye ni mhuni, basi aachane na mambo ya umma. Akaendeleze uhuni wake nje.

Lakini kuna hili pia: Kuonyesha huyu Selasini, ni muongo wa kupindukia, ni madai yake kwamba yeye ndiye aliyewapokea Anthony Komu na Mbatia, ndani ya mageuzi. Siyo kweli.

Mbatia na Komu, wamejiunga na NCCR- Mageuzi, kabla ya chama hicho, hakijawa chama cha siasa. Ni wakati ule, kikiwa kamati ya kudai mfumo wa vyama vingi – National Committee for Constitution Reform.

Kuthibitisha hili, Komu alikuwa mmoja wa watu waliotoa mada kwenye kongamano la kudai mfumo wa vyama vingi, lililoanzisha kamati hiyo, ambalo lilifanyika Diamond Jubilee,  tarehe 11 na 12 Juni 1991.

Selasini hakuwapo kwenye mkutano huu. Hakuwa mmoja wa waliotetea ujio wa vyama vingi. Sasa yeye aliyekuja baadaye, anawezeje kuwapokea watu ambao ni waanzilishi?

Wakati wenzake wanapigania ujio wa vyama vingi, Selasini alikuwa mtumishi katika iliyokuwa Benki ya Nyumba (THB). Alijiungia na chama hicho, mwaka 1992. Hapa tayari vyama vilikuwa vimeshaanzishwa na Komu na Mbatia wameshakuwa wanachama.

Ndio maana Komu alipewa kadi namba saba na Mbatia akawa na kadi namba sita. Yeye aliingizwa kwenye chama na Haidary Maguto, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara) na Mbatia. Ni baada ya kumfuata ofisi kwake THB.

Selasini aitaje namba ya kadi yake ya NCCR- Mageuzi, kabla hajaondoka na kujiunga na Chadema, ili tupime ukweli wa maneno yake.

Kile ambacho hataki kukieleza; na au watu kukifahamu ni hiki: Aliyemshawishi kuondoka NCCR-Mageuzi na kujiunga na Chadema, ni Komu.

Aliyemnunulia vifaa vya kampeni mwaka 2010, kwa thamani ya Sh. 750,000 (laki saba na elfu hamsini), ni Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema.

Ni Mbowe aliyelipia vifaa hivyo aina ya Ahuja – Public  Address System – kutoka mfukoni mwake katika duka la General Micro, lilipo mtaa wa Kitumbi, Dar es Salaam.

Bali, ni Selasini huyu huyu aliyemgeuka Mbowe na kumsingizia kwa mambo kadhaa, ikiwamo ubinafsi.

Katika barua yake kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, amedai kuwa Mbowe ni mtu wa kutumia wenzake kwa manufaa yake. Amesahau kuwa Mbowe huyo huyo, ndiye aliyemfikisha hapo alipo hadi kuitwa mbunge. Sijui anaposema kutumia wenzake, anakuwa na maana gani!

Hataki kusikia pia kuhusu Lamwai. Anajua nini alichomfanyia ndugu yake huyo wa damu. Hata madai kuwa vijana walimkataa katika uchaguzi wa ndani ya chama mwaka 2000, hayana ukweli.

Komu na vijana wengine kadhaa, akiwamo Mpelwa Lujiko Kalungubale, hawakumuunga mkono Mbatia. Walimunga mkono Mabere Nyaucho Marando.

Ni yeye, Mpita Bakana na Haji Ambari, ndio waliokuwa na Mbatia.

Hata hivyo, hata kama kutomuunga mkono Lamwai siyo kosa, lakini hakupaswa kumshambulia kwa matusi, kejeli, kumchonganisha na familia yake na mengine mengi ambayo hayawezi kuandikika.

Selasini anayajua haya. Anajua kuwa huo ndio msingi mkuu wa Dk. Lamwai, kushindwa kumsamehe mdogo wake wa damu, hadi mauti yanamfika.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Potofu huzaa potoshi/ potoshi huzaa potofu?

Spread the loveDayosisi 7 za KKKT katika kanda ya Ziwa na Magharibi,...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo

Spread the loveWAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kuwa kinara wa demokrasia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mabeyo ametuepusha

Spread the loveNIMEGUSWA na uadilifu, utiifu na uaminifu wa Mkuu mstaafu wa...

error: Content is protected !!