July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Joseph Haule: Ubunge hautaniondoa kwenye muziki

Spread the love

MSANII mkongwe wa muziki wa Bongo fleva nchini Joseph Haule maarufu kama Prof. Jay ameiambia Mwanahalisi online kuwa hataacha muziki kamwe kwani ni kipaji alichopewa na Mungu. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Prof. Jay ambeye pia kwa sasa ni mbunge mteule katika Jimbo la Mikumi Mkoani Morogoro kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) amesema hayo kwa njia ya simu alipozungumza na mwandishi.

Haule amethibitisha kuwa muziki ni sehemu ya maisha yake hawezi kuwaacha mashabiki wake hata baada ya kuwa mbunge.

Mbunge huyo mteule amesema, wananchi wa Mikumi wasiwe na wasi wasi kwani ana uwezo wa kuwatumikia wananchi wake huku akiendelea na muziki japo hatakuwa kwenye chati na ushindani kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

“Kuwa mbunge sio kifungo kwamba hutakiwi kufanya mambo yako binafsi. Mbona kuna wachungaji ni wabunge lakini wanafanya kazi zao kama kawaida. Naahidi kuwatumikia wananchi wangu kwa nguvu zangu zote kama nilivyoahidi na kuifikia Mikumi mpya tunayotaka”. Amesema Prof.Jay.

Prof. Jay alishinda kwa kishindo Jimboni humo kwa kumbwaga mpinzani wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jonas Nkya ambapo Prof. Jay alipata kura 32259 na mpinzani wake kura 30425 hivyo kutangazwa kuwa mbunge kwa tofauti ya kura 1834 dhidi ya mpinzani wake.

Mbali na hilo, Prof. Jay amewashukuru wapiga kura wake wa Mikumi kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo ambapo amewaahidi kuwatumikia kwa kutumia muda mwingi kuwa Jimboni kwake na kufanya kazi kwa ajili ya wananchi kuliko kufanya muziki kiushindani kama ilivyokuwa mwanzo.

Prof. Jay amewahi kutamba na nyimbo nyingi kama ndio mzee, kipi sijaskia, nikusaidieje? Na nyingine nyingi za kiharakati ambazo pia zinaweza kuwa zilimuongezea umaarufu wake na kumfanya apendwe zaidi kutokana na harakati zake kwenye siasa.

error: Content is protected !!