KAMPUNI ya Johnson & Johnson kutoka nchini Marekani imesitisha majaribio ya chanjo ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) Barani Afrika baada ya chanjo hiyo kushindwa kuonesha matokeo mazuri. Anaripoti Gabriel Mushi, Dar es Salaam … (endelea).
Chanjo hiyo iliyoanza kutolewa mwaka 2017 kwa baadhi ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe, ilitolewa kwa wasichana 2,600.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 31 Agosti, 2021na kampuni ya Johnson & Johnson kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati Tendaji na Ofisa Mkuu wa Sayansi wa kampuni hiyo, Dk. Paul Stoffels, amesema ni jambo la kusikitisha kwamba majaribio ya chanjo hiyo yameshindikana licha ya ugonjwa huo kuathiri zaidi ya watu milioni 38 duniani.
Amesema majaribio ya chanjo hiyo iliyopewa jina la Imbokodo au kisayansi HVTN 705/HPX2008 ulikuwa ni mpango wa ushirikiano kati ya kampuni ya Johnson&Johnson, Kampuni ya dawa kutoka Marekani – Bill & Melinda Gates Foundation na Serikali ya Afrika Kusini.
“Wanawake wasiopungua 2,600 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 kutoka Malawi, Msumbiji, Zambia, Afrika Kusini na Zimbabwe, walishiriki katika jaribio hili.
“Licha ya kwamba na nusu yao walipokea sindano nyingi za chanjo hiyo ya majaribio, miaka miwili baada ya sindano ya kwanza, matokeo yalionekana hayafai… hata kama chanjo hiyo ilitumiwa vizuri, ufanisi wake ni wa asilimia 25 tu!,” amesema Dk. Stoffels.
Aidha, Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu Mtendaji wa Baraza la Utafiti wa Tiba nchini Afrika Kusini (SAMRC), Profesa Glenda Gray ambaye pia ni Mwenyekiti wa mpango huo wa chanjo ya Imbokodo, amesema janga la maambukizi ya VVU bado ni changamoto kubwa Afrika.

“Asilimia kubwa ya vijana na wanawake kusini mwa Afrika ndio waathiriwa wakubwa wa ugonjwa huu, licha ya maendeleo makubwa yaliyopatikana katika matibabu na kinga ya VVU.
“Bado ni changamoto kubwa kiafya ukanda huu, hii inatutaka kutumia maarifa yatakayopatikana kutoka kwenye majaribio haya kuendeleza utafiti wa chanjo ya VVU duniani,” amesema.
Kufuatia majaribio ya chanjo hiyo kubuma, Johnson&Johnson imesema inaendelea awamu ya tatu ya mpango wa majaribio ya chanjo nyingine ya VVU kwa wanaume wanaojamiiana na wanaume wenzao katika ukanda wa Amerika ya Kusini.

IMBOKODO NI NINI?
Imbokodo ni neno lililotoholewa kutoka katika lugha ya kabila la Zulu huko Afrika Kusini.
Imbokodo maana yake ni jiwe au mwamba. Neno hilo limetokana na nahau kutoka katika kabila hilo inayosema kwamba “Ukimpiga mwanamke, Umempiga mwamba”
Leave a comment