Friday , 9 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa John Shibuda: Muswada wa vyama unamchafua Rais Magufuli 
Habari za SiasaTangulizi

John Shibuda: Muswada wa vyama unamchafua Rais Magufuli 

Rais John Magufuli
Spread the love

KATIBU Mkuu wa chama cha ADA-TADEA, John Magale Shibuda, amedai kuwa muswada mpya wa vyama vya siasa uliowasilishwa bungeni na serikali, umelenga “kuichafua taswira nzuri ya Rais John Pombe Magufuli, mbele ya uso wa dunia.” Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Shibuda alisema, “muswaada huu, ni adui mkubwa kwa Rais Magufuli. Muswaada unalenga kumgombanisha rais na wananchi wake” na kuonya, “tafadharini musimpeleke huko.”

Akiongea kwa hisia kali, huku akimtolea macho Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Shibuda alisema, Rais Magufuli amekuwa na rekodi nzuri ya kulijenga taifa hili kiuchumi. Amejijengea jina kimataifa, lakini muswaada unataka kumchafua.

Aidha, Shibuda alidai kuwa muswaada uliyopo mbele ya Kamati, anaufananisha na jinsi Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilivyolitokomeza Azimio la Zanzibar.

Alisema, “…mheshimiwa mwenyekiti wa Kamati, Muswada uliyopo mbele yako, naufananisha na mkakati wa CCM na serikali yake wa kulitokomeza Azimio la Arusha na kuzalisha Azimio la Zanzibar. Hii ni kwa sababu, muswaada unavinyang’anya vyama vya siasa fursa muhimu ya kukuwa na kujiimarisha.”

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, badala ya muswaada kusaidia kukuza vyama, unalenga kuvidhoofisha vyama hivyo.

Shibuda ambaye alianza mchango wake kwa kunukuu misemo na maandishi kadhaa, ikiwamo yale ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na yale ya baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini.

Miongoni mwa misemo na maandishi ambayo Shibuda aliyanukuu, ni pamoja vitabu vya Mwalimu Nyerere vya Tujisahihishe, Nyufa za Uongozi na Hatma ya Tanzania. Alitaja pia kauli ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa kwenye mkutano mkuu wa chama chake (CCM) mwaka 1992.

 

Vile vile, alitoa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Zanzibar; waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC); Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na andishi la baraza la vyama vya siasa kwa Kamati hiyo ya Bunge.

Akizungumzia ushiriki Baraza la Vyama vya Sisasa katika kuandaa rasimu ya muswaada na hadi kuufikisha bungeni, Shibuda alisema, baraza hilo ambalo yeye ni mwenyekiti wake, halikushirikishwa katika hatua hizo.

Alimtuhumu Jaji Francis Mutungi, kulivuruga baraza hilo. Alidai kuwa kwa maoni yake, muswaada umeletwa bungeni kinyume na utaratibu.

Alisema, “tunayo malalamiko mengi kuhusu muswaada huu. Moja ni kwamba sisi katika baraza la vyama vya siasa, hatukushirikishwa katika jambo hili. Baraza limenyang’anywa fursa hiyo na msajili Jaji Mutungi kwa kutufutia mwaliko ambao tayari ulishatolewa na spika.”

Aliongeza, “naomba kuweka rekodi sawasawa. Kwamba, baraza halikupewa nafasi ya kujadili muswaada huu.”

Kwa siku  mfululizo – Jumamosi na Jumapili, Kamati ya Katiba na Sheria, ilipokea maoni ya viongozi wa vyama vya siasa juu ya muswada wa sheria ya vyama vya siasa Na. 4 wa mwaka 2018.

Kabla ya vyama kutoa maoni yao, kamati ilikutana na wadau wengine, wakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali; taasisi za kidini, vyuo vikuu na watu binafsi.

Akizungumza mbele ya kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Jeremia Mtobyesa, ambaye ni wakili wa mahakama kuu na mjumbe katika bodi ya uongozi ya chama cha wanasheria Tanganyika (TLS), alidai kuwa sheria inayotaka kutungwa kupitia muswaada huo, “imesheheni vimelea ya udikteta.”

Amesema, baadhi ya vifungu vilivyomo kwenye muswada vinapingana na katiba ya nchi. Ametoa mfano wa kifungu kinachotoa kinga kwa msajili wa vyama na vile vinavyozuia watu kukata rufaa.

Mtobyesa amesema kuwa katika taifa hili, kila taasisi kumewekwa utaratibu wa kukata rufaa. Akaongeza, “kutoruhusu ukataji wa rufaa kama ambavyo sheria inayotungwa inavyotaka, ni kinyume na katiba.”

Baadhi ya wajumbe wa kamati walihoji uelewa wa waliotoa maoni, kufuatia baadhi ya wasilishaji kushindwa kufanya uchambuzi,  na badala yake, wakaishia kunakiri muswada ulioletwa kama ulivyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaTangulizi

Ngoma bado mbichi mkataba wa Bandari

Spread the love  SAKATA la mkataba wa uendeshaji, uendelezaji na uboreshaji wa...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mkataba unaweza kuvunjwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mikataba ya utekelezaji bado haijasainiwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

Habari za Siasa

Lussu: Mkataba wa DP bandarini si wa miaka 100

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema hakuna ukweli wowote...

error: Content is protected !!