January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JKT wachafuliwa kupitia mavazi yao

Spread the love

JESHI la Polisi wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma linamshikilia mtu mmoja ambaye alikutwa amevaa sare za jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Kijana huyo ambaye jina lake halijafahamika siku ya Ijumaa usiku alikutwa katika maeneo ya Hazina Mpwapwa akiwa amevaa kombati hizo huku akiwatishia wananchi kuwa ni mwanajeshi.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Rafael Mahundi aliliambia gazeti hili kuwa mtu huyo alikuwa akitumia sare hizo kuwatishia watu hususani wafanyabiashara kwa kutaka wampe fedha au bidhaa.

Mahundi amesema kwamba eneo lingine ambalo alikuwa akifanyia utapeli ni katika maeneo ya baa ambapo alikuwa akilazimisha kupata pombe ya bure.

Mtoa taarifa huyo amesema baada ya wananchi kumshutukia walitoa taarifa polisi akiwa maeneo ya Hazina.

Amesema majira ya saa tatu usiku juzi jeshi la polisi lilimkamata mtu huyo na kumweka ndani.

Hata hivyo taarifa za uhakika kutoka jeshi la polisi wilayani Mpwapwa zinaweka bayana kutokea kwa tukio hilo.

Mmoja wa askari wa cheo cha chini amesema mtuhumiwa huyo alifikishwa kituoni hapo Ijumaa usiku lakini alipewa dhamana na askari wa kike siku ya Jumamosi saa tatu.

“Kweli siku ya Ijumaa usiku alikamatwa mtu ambaye alikuwa na sare za JKT ambazo alikuwa akizitumia kuwatishia wananchi hususani wafanyabiashara wakiwemo wafanyabiashara ya kuuza pombe.

“Ila jambo la kushangaza siku ya Jumamosi saa tatu usiku alipewa dhamana na askari wa kike (jina linahifadhiwa) lakini baada ya suala hilo kufika mkoani kijana huyo amekamatwa tena na kurudishwa mahabusu,” amesema mtoa taarifa hiyo.

Kwa upande wake mkuu wa polisi mkoa wa Dodoma, David Misime alipotafutwa kwa njia ya simu, amesema kwamba analifuatilia jambo hilo.

“Ngoja nifuatilie si unajua utaratibu wangu wa kutoa taarifa nikisha kamilisha nitawaambia,” amesema Misime.

error: Content is protected !!