November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JKCI yasaini mkataba na Poland kutibu moyo

Spread the love

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imesaini mkataba wa ushirikiano na chuo Kikuu cha Jagiellonian nchini Poland, wenye lengo la kubadilishana ujuzi wa utoaji wa huduma za matibabu ya kawaida na upasuaji wa moyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mkataba huo utakaoanza kutumika mapema mwakani, ulisainiwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian, Prof. Bartlomiej Guzik.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kusaini mkataba huo, Dk. Kisenge alisema, mkataba uliosainiwa umelenga kuongeza wigo katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo pamoja na upasuaji wa moyo katika taasisi yake.

“Tumesaini makubaliano ambayo yatawawezesha wataalam wetu kwenda nchini Poland, kujifunza namna wenzetu wanavyotoa huduma za magonjwa ya moyo.

“Mkataba unaruhusu pia wataalamu wa Poland kua nchini, kuona na kujifunza jinsi tunavyotoa huduma za tiba na upasuaji wa moyo,” ameeleza.

Aidha, Dk. Kisenge alisema, kupitia ushirikiano huo, wamekubaliana na chuo hicho kuleta wataalam wao watakaoshirikiana nao katika kuwahudumia wagonjwa wa moyo.

Miongoni mwa maeneo ambayo watajikita nayo, ni upasuaji wa moyo hasa kuzibua mishipa ya damu iliyoziba, kubadilisha valvu za moyo bila kupasua kifua kupitia upasuaji unaoitwa, “TAVI Procedure” ambao haujaanza kufanyika nchini.

Kwa mujibu wa Dk. Kisenge, mkataba huo umeongeza wigo wa JKCI kuwa na ushirikiano na mashirika yanayotoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo hadi kufikia 18 kwa sasa.

 Hakuyataja mashirika mengine ambayo yanashirikiana na JKCI katika kushughulikia tatizo la moyo nchini.

Lakini alisema, “tutaendelea kuongeza ushirikiano huu wa kubadilishana uzoefu na nchi nyingine ambazo tunaamini zinatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo, kwa lengo la kuifanya JKCI kuwa bingwa wa magonjwa ya moyo Afrika.”

Naye Guzik – makamu mkuu wa chuo kikuu cha Jagiellonian – alisema, wamevutiwa kufanya kazi na wataalam wa afya wa JKCI ili kwa pamoja, waweze kutoa huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Alisema, “kujenga uhusiano baina yetu na JKCI kutasaidia kuboresha huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa moyo lakini pia kutaongeza ubobezi kwa wataalam hawa wa afya.”

error: Content is protected !!