September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

JK: ‘Nilimpaisha’ Diamond

Spread the love

DK. Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu amesema kuwa, yeye ni miongoni mwa ‘waliompaisha’ Nasibu Abduli maarufu kwa jina la Diamond Platinum, anaandika Dany Tibason.

Amesema, akiwa madarakani amemsaidia kumuunganisha na wasanii wa nje jambo lililomuwezesha kufanya kazi nao na kukishauri Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutowatenga wasanii kwa kuwa wamekuwa wakitoa mchangi wao kwenye chama hicho.

“…mimi niliwapenda sana wasanii, niliwasaidia hadi wengine kama kina Diamond Platinum kufanya kazi na wasanii wa nje na wasanii wengi wameona mafanikio ya kazi zao,” amesema Rais Kikwete.

Ameusisitiza uongozi mpya wa CCM kufanya kazi na wasanii waliopo nchini kwa kuwa, hatua hiyo haitakipotezea chama mwelekeo.

“Kinana (Abdulrahman Kinana-Katibu Mkuu CCM) jambo ambalo halitawapotezea mwelekeo ni kufanya kazi na wasanii,” amesema Kikwete.

Ametoa kauli hiyo juzi katika hafla ya usiku wa wasanii iliyoandaliwa na wasanii hao kwa ajili ya kumuaga baada ya kukabidhi uenyekiti wa CCM kwa Rais Dk. John Magufuli.

Amesema, katika uongozi wake alishirikiana na wasanii kwa kuwa, ilikuwa ni rahisi kutuma meseji ya kitu alichokisema kwa haraka.

“Kwa kutambua umuhimu wa wasanii, nilianza kujaribu maji kwa wasanii kwa kuwa nao katika shughuli mbalimbali na kuwasaidia ili waone thamani ya kazi yao,” amesema na kuongeza;

“Kwa chama cha siasa kuwa karibu na wasanii ni vizuri kwa maslahi ya chama na kwamba, chama hiki kilitumia sana nguvu za wasanii.”

Baadhi ya wasanii waliopata nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wenzao, wamesema, hawatamsahau Rais Kikwete kwa kuwa amewasaidia wengine kujenga nyumba hata kumiliki magari kutokana na kazi wanazozifanya.

Jacob Steve (JB) amesema, kitendo cha Rais Kikwete kuwa nao kiliwafanya waheshimike na kuwafanya watu wawajue na kuwapa kiburi kuwa nao ni watu katika jamii.

Amesema kuwa, wasanii wapo sambamba na Rais Magufuli katika ukusanyaji mapato na kwamba, wataendelea kushirikiana na chama na serikali katika shughuli mbalimbali.

Kinana amesema, maneno yaliyozungumzwa na wasanii si maneno tu bali yana ujumbe mzito kwa chama na serikali na kuahidi kujifunza kufuata nyayo za Rais Kikwete.

error: Content is protected !!