August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JK, Lowassa gumzo msiba wa Masaburi

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Spread the love

KUKUTANA ana kwa ana kwa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa katika hafla ya kuuaga mwili wa Dk. Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kumeacha gumzo, anaandika Wolfram Mwalongo.

Wawili hao walikutana jana kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu Julai mwaka jana baada ya jina la Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete ndio walikuwa wa kwanza kuwasili katika viwanja hivyo na kukaa msatari wa mbele.

Baada ya muda mchache Lowassa akiambatana mkewe Mama Regina Lowassa waliwasili na kwenda moja kwa moja kukaa mstari wa tatu alikokuwa ameketi Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM.
Kikwete aligeuka nyuma na kumwona Lowassa ambapo alimfuata na kumpa mkono na wote wakionesha uso wa tabasamu.

Tangu Lowassa alipoingia kwenye viwanja hivyo, waombolezaji walikuwa wakiwakodolea macho wote wawili (Lowassa na Kikwete) na kutamani kuona kama watasalimiana.

Hatua ya Kikwete mwaka jana akiwa mwenyekiti wa CCM kusimamia kuenguliwa kwa jina la Lowassa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM, kulimsukuma kuondoka kwenye chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Baada ya kujiunga na Chadema na kupitishwa kugombea urais, Lowassa aliungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa unaundwa na vyama vinne ambavyo ni Chadema yenyewe, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na NLD.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana Lowassa alipata kura 6,072,848 akitanguliwa na Dk. John Magufuli aliyepata kura 8,882,935.

Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Rais Kikwete ambaye baadaye walijikuta wametumbukia kwenye uhasama mkubwa wa kisiasa jambo lililosababisha kubadili taswira ya kisiasa ndani ya CCM kutokana na kuibuka makundi mawili makubwa.

Tukio la wanasiasa hao kukutana kwenye msiba huo liliteka hisia za mamia ya ndugu, jamaa na marafiki waliofika kwenye viwanja hivyo kutoa heshima zao za mwisho kwa Masaburi kutokana na kuwa na uhasama wa kisiasa.

Uhasama wa wawili hao ulichipuka baada ya Lowassa kuamua kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya Richmond na kukomaa baada ya jina lake kuenguliwa.

error: Content is protected !!