January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JK atangaza vita watakaosubiri matokeo vituoni

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete ametangaza vita na wapigakura watakaobakia maeneo ya vituo vya uchaguzi baada ya kupigakura zao, akisema watakuwa wanavunja sheria za nchi. Anaandika Charles William … (endelea).

Akiwa ni Amiri Jeshi Mkuuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, Rais Kikwete ameonya kwamba watakaokaa vituoni ‘watashughulikiwa’ na serikali. 

Ametoa tamko hilo mchana leo alipokuwa akihutubia kilele cha mbio za mwenge wa uhuru kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa.

Rais ambaye dhahiri ametoa majibu ya kilichojitokeza kuwa ni malumbano yanayoendelea kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jeshi la Polisi na Serikali kwa upande mmoja na kwa upande wa wili viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Wakati Tume na serikali wamekuwa wakisisitiza kuwa wananchi hawatakiwi kukaa maeneo ya karibu na vituo vya uchaguzi baada ya kupiga kura, viongozi wa UKAWA – Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD – wanahimiza watu kubakia vituoni masafa ya mita 100 nje ya vituo kwa ajili ya kujiandaa kulinda kura za wagombea wao.

Oktoba mosi mbele ya umati mkubwa wa wananchi kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, “mkishapiga kura, wanawake nendeni nyumbani, wanaume mtakaa umbali wa mita 200 unaotakiwa kisheria na mtakaa hapo mkilinda kura zenu mpaka matokeo yatakapopatikana.”

Viongozi wa UKAWA wanasema kwamba hakuna haki kwa wananchi kuambiwa waende kusubiri matokeo ya uchaguzi majumbani kwao wakati kuna dalili nyingi za kutokuwepo uhakika kuwa Tume itamudu kuzilinda kura dhidi ya kuchakachuliwa.

Tume ya Uchaguzi imekuwa ikijitahidi kuonesha uwazi katika mifumo ya ushughulikiaji kura ingawa imekataa katakata kuonesha mifumo ya ujumlishaji wa kura wakati daftari lenyewe imelitoa jana kwa ajili ya kuhakikiwa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi.

Katika hali hiyo ya malumbano, Rais Kikwete anajitokeza kusema kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote anayekusudia kuvunja sheria kipindi cha uchaguzi kwa kuwa hayuko tayari kuona demokrasia “inatekwa nyara.”

Rais analalamika kwa kuhoji, “Mnakaa nje ya vituo vya kupigia kura kufanya nini? Wewe upo nje ya kituo, utalindaje kura? Mtu wa kulinda kura ni wakala wa chama chako, labda kama ni mzembe.”

“Mipango ya kuvuruga amani inafahamika na itadhibitiwa watu wao wapige kura mapema na wanawake waende nyumbani, wanaume wabaki kulinda kura, wanadhani wengine hawawezi kuwahi… msiilazimishe serikali kufanya mambo yasiyopendeza, wanaotaka kufanya fujo hawatavumiliwa waatadhibitiwa,” amesema.

“Mkishapiga kura nendeni nyumbani Tume ya Uchaguzi imeshafafanua vizuri suala hili… tofauti na hapo ni vurugu, na sisi kama serikali hatutawavumilia watakaokiuka sheria. Tutawadhibiti kwa nguvu ileile watakayoitumia,” amesema katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa amedai suala la kulinda kura ni mkakati wa viongozi wa vyama vya siasa kuwazuia baadhi ya wananchi kupigakura baada ya wanachama wa vyama vyao kupiga kura.

Huko nyuma, viongozi wa UKAWA walishatangaza kuwa watayatangaza matokeo ya kura za urais hata kabla ya Tume, kwa kuwa sheria inaruhusu kutangaza kura zinazokamilika kuhesabiwa na kuidhinishwa na wagombea na mawalaka wao almuradi sio matokeo ya majimbo yote.

error: Content is protected !!