August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JK ataka mikutano ya hadhara

Spread the love

JAKAYA Kikwete, Rais mstaafu wa awamu ya nne na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyemaliza muda wake, amewataka viongozi wa chama hicho kufanya mikutano ya hadhara kote nchini ili kukiimarisha chama hicho, anaandika Regina Mkonde.

Kikwete ameyasema hayo leo wakati akitoa hotuba yake katika mkutano maalumu wa chama hicho wa kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa chama hicho Taifa.

“Viongozi wetu kutofanya mikutano kwa wananchi ndiyo sababu mambo yalianza kutuharibikia huko nyuma na hatutaki iwe hivyo tena, naomba mwenyekiti ujaye wa chama, usiache hii hali iendelee.” Amesema Kikwete huku akiongeza;

“Viongozi wakienda kwenye mikutano ya hadhara hushangaa namna wananchi wanavyojitokeza kwa wingi kuwasikiliza, kwa nini mnaogopa kwenda kwa wananchi, kama tunawatafuta wanachama wapya hivi tutawapataje bila kwenda walipo?” amehoji Kikwete.

Rais mstaafu Kikwete pia amempongeza katibu mkuu wa chama hicho Kanali mstaafu Abdurahman Kinana kwa kuendesha mikutano mingi ya hadhara ili kufufua uhai wa CCM katika kipindi chote cha miaka mitatu kama katibu mkuu wa chama hicho.

“Nampongeza Kinana kwani katika kipindi chake, amekuwa nguzo imara ameenda katika mikoa, wilaya na majimbo yote hapa nchini kuzungumza na wananchi na alifika mpaka maeneo ambayo viongozi wa chama huko hawakuwahi kufika. Amesema Kikwete.

Amesisitiza kuwa viongozi wa chama hicho kutokwenda kwa wananchi na kufanya mikutano ni miongoni mwa sababu za CCM kuyumba na kuwa na wakati mgumu wa kupata kura za wananchi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kauli hii ya Kikwete imekuja leo, ikiwa ni miezi michache tangu kutangazwa kwa marufuku ya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ambayo ilitangazwa na Rais Magufuli na kutiliwa mkazo na Jeshi la polisi hapa nchini.

Ni marufuku hiyo ya mikutano ya hadhara ndiyo iliyosababisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo kupitia Naibu Katibu Mkuu wake (Bara) John Mnyika kufungua kesi mwanzoni mwa juma hili katika mahakama ya haki ya Afrika Mashariki kupinga zuio hilo la serikali.

Wito wa Rais mstaafu Kikwete kumtaka Rais Magufuli kuendeleza utamaduni wa viongozi wa CCM kufanya mikutano ya hadhara imetafsiriwa kama ukosoaji wa wazi dhidi ya marufuku ya serikali na Jeshi la Polisi juu ya mikutano hiyo hapa nchini.

 

error: Content is protected !!