January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

JK aongeza ahadi kwa walimu

Rais Jakaya Kikwete (katikati) akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania. Kushoto ni Rais wa Walimu, Gratian Mukoba. Kulia ni Waziri wa Ajira na Kazi, Gaudencia Kabaka

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete amewaahidi walimu kuwa watarajie nyongeza ya mishahara itakayoanza Agosti mwaka huu, ikiwa ni moja kati ya jitihada za Serikali katika kuboresha maslahi yao. Ferdinand Shayo, Arusha … (endelea).

Ahadi hiyo, ameitoa jijini Arusha wakati akihutubia mkutano mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), akisema nyongeza hiyo itahusisha walimu wote wanaolipwa kima cha chini na cha juu pasipo kutaja kiwango kilichoongezeka.

“Wakati mnachukua mishahara yenu benki Agosti, mtaona tofauti ambayo ni nyongeza ya msahara, wenzenu wa chama cha wafanyakazi waliniomba nisitangaze, niongeze kimya kimya ili wafanyabiashara wasipandishe bei ya bidhaa,” amesema Kikwete

Amesema serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha inaboresha elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya walimu, kuongeza vifaa vya kujifunzia na kufundishia, nyumba za walimu, vitabu na maabara.

Kikwete ameendelea kuahidi kuwa madai ya walimu yatalipwa kwa awamu na kwamba iwapo uhakiki utakamilika kwa sasa, wanatarajia kulipa kiasi cha Sh. 7 bilioni kwa walimu 70,100 ifikapo Agosti mwaka huu.

Sehemu ya walimu waliohudhuria mkutano huo
Sehemu ya walimu waliohudhuria mkutano huo

“Katika kufanya uhakiki wa madai ya walimu ikiwemo malimbikizo ya mishahara, posho za kufundishia na uhamisho, tuligundua kuwa wako baadhi ya watu walifanya udanganyifu lakini sasa tunamalizia uhakiki ili fedha hizo zilipwe,” amesema Kikwete.

Naye Katibu Mkuu wa CWT, Alhaji Yahaya Msulya, amemtaka Rais Kikwete kushughulikia suala la posho ya kufundishia kwa walimu kwani wao ni kundi linalofanya kazi kwa muda mrefu kuliko watumishi wengine wa serikali.

“Mwalimu anaingia shuleni saa 1:30 asubuhi, anatoka saa 3:00 muda huo anatakiwa kusahihisha kazi za wanafunzi na kuandaa masomo ya kufundishia kesho, hivyo anatumia muda mwingi sana katika kazi, ni vyema serikali ikaliangalia suala hili,” alisema.

error: Content is protected !!