January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jinsi Zitto, Prof. Lipumba wanavyomzungumza JPM

Rais John Magufuli

Spread the love

 

VYAMA vya Siasa nchini Tanzania vimeungana na viongozi mbalimbali kutoa salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea jana tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akitangaza kifo cha Rais Magufuli jana tarehe 17 Machi 2021, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani alisema, kiongozi huyo wa Tanzania alifariki dunia akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo hospitali hapo.

Chama cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo vimetuma salamu zao za pole kwa familia ya Rais Magufuli na Watanzania kwa ujumla.

ACT-Wazalendo kupitia kiongozi wake, Zitto Kabwe, kimetoa pole kwa Rais mteule, Samia Suluhu Hassani kufuata msiba huo mzito.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Zitto amesema, Rais Magufuli atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Tanzania.

“Hayati Magufuli katika uhai wake amekuwa kiongozi wa nchi yetu katika nyadhifa mbalimbai na kwa hakika alitekeleza wajibu wake kwa juhudi kubwa, Taifa litamkumbuka kwa mchango wake kwenye maendeleo yetu,” amesema Zitto.

Naye Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema, taifa limegubikwa na giza nene kufuatia msiba huo.

“Mimi binafsi na CUF tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Kifo cha Rais Magufuli kilichotokea jana Machi 17, 2021 saa 12:00 jioni kutokana na maradhi ya moyo. Kwa hakika Taifa limegubikwa na huzuni kubwa na giza nene,” amesema Prof. Lipumba.

Amesema, Rais Magufuli atakumbukwa kwa jitihada zake za ujenzi wa miradi ya maendeleo hasa miundombinu.

“Masikio yamepokea taarifa ambayo akili haziko tayari kuibeba wala kuikubali kwa kuzingatia uhalisia, kwamba ni wiki tatu tu zilizopita marehemu Rais Magufuli alifanya kazi kubwa bila kuchoka, za kuzindua miradi mikubwa ya maendeleo,” amesema Prof. Lipumba na kuongeza:

“Kifo chake cha ghafla kinatia uchungu na simanzi kubwa. Amri ya Mungu haina makosa. Kila wakati kauli za Rais Magufuli zilimtanguliza Mwenyezi Mungu.

“Watanzania tutamkumbuka marehemu Dk. Magufuli kwa makubwa aliyoyafanya kwenye ujenzi wa miundombinu, kupambana na ufisadi kwa kiwango kikubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu na kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa serikali.”

Amesema, miradi iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais Magufuli ni pamoja na Daraja la Ubungo (Kijazi Interchange) na Stand Mpya ya mabasi iliyopo Mbezi, Dar es Salaam.

Nacho NCCR-Mageuzi kimesema “Tumepkkea kwa asikitiko makubwa taarifa za kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.”

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema katika kuomboleza kifo hicho, bendera za chama hicho zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa siku 21.

 

“Mwenyezi Mungu ameamua kufungua ukurasa mpya kwa nchi yetu. Salamu zetu za rambirambi zitatolewa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe. Naelekeza bendera zote zipepee nusu mlingoti kwa siku 21,” ameandika Mnyika katika ukurasa wake wa Twitter.

error: Content is protected !!