October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jinsi Askari Magereza alivyoua binti mahakamani

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa

Spread the love

NEEMA Andrew (umri 22-25) ameuwawa kwa kupigwa risasi na Askari Magereza ndani ya viwanja vya Mahakama ya Kigamboni jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Hakuwa mtuhumiwa wala kutenda kosa lolote lakini uhai wake ulikatizwa na askari huyo aliyekusudia kumlenga mtuhumiwa aliyeachwa huru na mahakama.

Taarifa zaidi zinaeleza, Askari Magereza huyo alikuwa akimlenga mtu mmoja aliyekuwa mtuhumiwa mahakamani hapo na kuwa, alidhani anatoroka.

Mtuhumiwa huyo (hakutajwa jina) alikuwa ameachwa huru na mahakama lakini Askari Magereza huyo hakujua kama mtu huyo ameachwa huru.

SACP Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam akizungumza na MwanaHALISI ONLINE leo amesema, taarifa za kupigwa risasi kwa binti huo anazo.

Kamanda Mambosasa amefafanua kuwa, aliyehusika kwenye tukio hilo ni dereva wa Askari Magereza na kwamba, alifyatua risasi ili kumkamata mtu aliyedhani kwamba ni mtuhumiwa aliyetoroka mahakamani.

Binti huyo alipigwa risasi na kufariki dunia juzi tarehe 20 Februari 2019 huku mama yake Halima Abdallah akijeruhiwa na risasi hiyo. Kwa sasa Halima amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke.

Baada ya tukio hilo, taarifa zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana ambapo ilidaiwa, aliyefanya tukio hilo ni askari polisi wa Kituo cha Polisi cha Kigamboni jambo ambalo Kamanda Mambosasa amepinga.

“Aliyepiga risasi hakuwa askari polisi, alikuwa dereva wa askari magereza, alidhani mshtakiwa ametoroka kumbe alikuwa ameachiwa huru, wao wakadhani ametoroka. Kwa bahati mbaya risasi hiyo ikampata binti huyo,” amesema Kamanda Mambosasa.

Amesema, kwa sasa dereva huyo anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kigamboni akituhumiwa kwa kosa la kuuwa pasipo kukusudia.

Kuhusu mama wa marehemu Neema-Halima Abdallah- Kamanda Mambosasa amesema, anaendelea kupatiwa matibabu ya jeraha alilompata kwenye paja katika Hospitali ya Temeke.

error: Content is protected !!