August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jiji la Mwanza tuhumani

Jiji la Mwanza

Spread the love

HALMASHAULI ya Jiji la Mwanza imeingia katika mvutano mkali wa kugombea ardhi na wananchi wa Mtaa wa Nyabulogoya, Kata ya Nyegezi Wilaya ya Nyamagana, anaandika Moses Mseti.

Mgogoro huo wa ardhi ulioanza mwaka 2013, umesababisha wananchi wa mtaa na kata hiyo kukosa huduma za kijamii ikiwemo vituo vya afya kutokana na uongozi wa jiji hilo kuuza viwanja hivyo kwa watu wengine.

Viwanja hivyo vilivyopo katika mtaa huo vilitengwa kwa ajili ya kujengwa shule ya msingi na sekondari, eneo la makaburi, soko, zahanati na maeneo mengine ya wazi kwa ajili ya shughuli zingine ambapo jiji hilo, limeuza viwanja hivyo vyenye ukubwa zaidi ya heka 30.

Keffa Otieno, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyabulogoya, Kata ya Nyegezi Wilaya ya Nyamagana akitoa kilio chake jana mbele ya John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza pamoja na Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza amesema, jiji lilipima eneo hilo mwaka 2000 kwa ajili ya matumizi hayo.

Mwenyekiti huyo amesema, wakazi wa maeneo hayo wamekosea huduma mbalimbali ikiwemo ya kituo cha afya kutokana na uongozi wa jiji hilo kuuza viwanja.

Amesema, wanapofuatilia suala hilo katika mamlaka husika, hupigwa kalenda.

“Mwaka 2000 walipoanza utaratibu wa kuuza maeneo hayo huku wakiwahamisha watu wengine na kuwalipa watu na wengine hawajalipwa mpaka sasa na tayari wameuza viwanja vyao kwa watu wengine, lakini hata huduma za kijamii zenyewe hakuna.

“Mkuu wa wilaya wa zamani wa Nyamagana (Baraka Konisaga) aliunda tume ya kuja kuchunguza suala hili, Julai 17 mwaka huu tume hiyo ilitakiwa kutoa ripoti lakini mpaka sasa hakuna majibu na tukiuliza na tunapowafuata wahusika (idara ya ardhi), wanatukimbika.

“Kiwanja namba 262 kilikuwa kwa ajili ya matumizi ya Shule ya Sekondari kimemilikishwa mtu, kiwanja namba 350 na 351 vilikuwa kwa ajili ya Kituo cha Afya na Kituo cha Polisi tayari vimeuzwa na kiwanja namba 170 kilichokuwa kwa matumizi ya uwanja wa mpira wa miguu,” amesema Otieno.

Otieno amesema kuwa, baada ya kuona uongozi wa jiji hilo ukiwapiga chenga kila kukicha, uongozi wa Serikali ya Mtaa uliamua kumuandika barua William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu suala hilo lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Mongella amesema kuwa, baada ya kusikia kilio hicho alimtaka mwenyekiti huyo (Keffa Otieno) kupeleka vielelezo vyote huku akiwataka watumishi wa idara ya ardhi jijini humo kuhakikisha wanatatua kero hiyo pamoja na kero za wananchi wengine.

Kibamba amesema kuwa, mgogoro huo anaufahamu na kwamba, atahakikisha linatatuliwa na kila mmoja anapata haki yake kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za ardhi bila kumpendelea mtu yeyote yule.

error: Content is protected !!