January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jiji la Mwanza kuonja ladha ya bomoabomoa

Spread the love

ADHA na mateso ambayo wamepata wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliofikiwa na bomoabomoa hivi karibuni, sasa inaelekezwa kwa wakazi wote wa halmshauri za jijini Mwanza, anaandika Moses Mseti.

Kauli hiyo imetolewa jana na Angelina Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa kikao kazi kilichowahusisha Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakurugenzi wa halmashauli na wakuu wa idara za mipango miji na ardhi jijini humo.

Angela amesema kuwa, wale waliodhani kwamba zoezi hilo ni kwa Dar es Salaam pekee wasahau kwani linatarajiwa kuanza katika kila halmashauri za Mwanza na sehemu zote nchini.

Angela amesema, kwa wale wote waliojenga nyumba zao katika maeneo hatarishi na yasiyokuwa rasmi wajiandae kisaikolojia kupokea zoezi hilo.

“Zoezi la bomoabomoa sio kwa Dar es salaam pekee, zoezi hili litazigusa halmashauli zote nchini na ni kwa maeneo ambayo ni mabondeni ambayo ni hatari kwa usalama wa binadamu,” amesema Angela.

Angela ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela jijini humo hakueleza siku na tarehe ya kuanza kwa zoezi hilo.

Pia amewataka wamiliki wa mashamba pori ambao hawayaendelezi wahakikishe wanayaendeleza mara moja na kwamba, kama itabainika kuna shamba halijaendelezwa litataifishwa na kugawiwa kwa wananchi.

error: Content is protected !!