December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jiji la Dodoma latenga bajeti ya Bil 180

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi

Spread the love

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepitisha bajeti ya Sh. 180 bilioni kwa lengo la utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa Mwaka ujao wa Fedha. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea). 

Bajeti hiyo inakusudia kumaliza baadhi ya changamoto zikiwemo zilizopo kwenye sekta ya elimu ambapo zimetengwa kiasi cha zaidi ya Sh. 8 bilioni.

Katika Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika jana katika ukumbi wa Jiji hilo, Baraza limepitisha bajeti hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2019/20 ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Godwin Kunambi aliwasilisha bajeti nzima mbele ya wajumbe wa baraza hilo lenye madiwani 60.

Kunambi alisema bajeti ya makusanyo yanayotokana na vyanzo vya ndani vya Halmashauri hiyo yanatarajiwa kuwa Sh. 72 bilioni, ikiwa imeongezeka kutoka Sh. 68 bilioni za mwaka huu unaondelea.

“Mheshimiwa Mwenyekiti na wajumbe, tukiangalia makusanyo yetu ya ndani kwa bajeti ya Mwaka tulionao sasa ni Sh. 68 bilioni, lakini kwa mwaka ujao tunatarajia kukusanya takribani Sh. 72 bilioni hivyo kuna ongeza la Sh. 5 bilioni,” alisema Kunambi.

Alisema moja ya vipaumbele katika mpango wa bajeti hiyo ni kuboresha sekta ya elimu ambapo jumla ya Sh. 8 bilioni zimetengwa.

Mkurugenzi Kunambi alisema Halmashauri anayoiongoza inakusudia kujitegemea na kujiendesha yenyewe kwa asilimia 100 kuanzia Mwaka 2021/22 ambapo itaachana kabisa na kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.

“Tunaposema Halmashauri kujitegemea na kujiendesha yenyewe maana yake ni kwamba tutatekeleza miradi ya maendeleo katika kata zetu kwa fedha za ndani, tutalipa mishahara ya watumishi wetu wote kwa fedha za ndani, pamoja na kulipa stahiki mbalimbali za watumishi tunakusudia kufikia hatua hii,” alifafanua.

Wakichangia hoja hiyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mstahiki Meya, Prof. Davis Mwamfupe walielezea kufurahishwa kwao na vipaumbele na ukubwa mpango na bajeti hiyo kwani wanaamini utaharakisha maendeleo kwa Wananchi wanaoowaongoza.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde alisema bajeti iliyopitishwa inagusa maisha na itaboresha sekta muhimu ikiwemo elimu, afya na maji.

“Bajeti hii kwenye elimu peke yake imetengwa zaidi ya Sh. 8 bilioni na hata ukiangalia kwenye sekta ya afya kiasi kilichotengwa ni Sh. 2 bilioni ambacho ni kiasi kikubwa sana, hii itasaidia kujibu kwa vitendo hoja za matumizi ya makusanyo makubwa tunayoyakusanya, hii ni bajeti ambayo kila anayeipenda Dodoma atakubali kuwa ni nzuri,” alisema Mavunde.

Mavunde alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo ya kwanza nchini kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuwezesha makundi maalum ikiwemo watu wenye ulemavu ambao katika bajeti hiyo wametengewa Sh. 3.3 bilioni ambazo zikitolewa kwa walengwa halmashauri itakuwa imefanya jambo kubwa la kupigiwa mfano.

“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi hili ni eneo langu la kazi kule serikalini na nafahamu changamoto ni kubwa kwenye uwezeshaji, tukienda katika kumbukumbu sisi tutakuwa halmashauri ya kwanza nchi nzima ambaye tumetenga fedha nyingi katika makundi haya maalum,” alisema Mavunde.

Kwa upande wake Mstahiki Meya Prof. Mwamfupe alisema bajeti ya hiyo ni yenye kuacha alama kwani haijawahi kutokea siku za nyuma na kwamba wamefikia hatua hiyo kutokana na juhudi na uzalendo wa Wanadodoma wote.

Alisema Jiji la Dodoma linatakiwa kuwa la mfano ili kuunga mkono juhudi kubwa za Serikali katika utoaji wa huduma za kijamii na kwamba ushirikiano na uzalendo kwa wadau ndiyo silaha pekee.

Naye Anselem Kutika ambaye ni Dwani wa Kata ya Kikuyu Kusini alisema anaunga mkono bajeti hiyo kwani haijawahi kutokea huku akitoa pongezi kwa wataalam wote wa Jiji wakiongozwa na Mkurugenzi Kunambi.

Bajeti iliyopitishwa na Baraza hilo jana inatarajiwa kuendelea kujadiliwa katika ngazi mbalimbali za juu kabla ya kuanza kutumika mapema Mwezi Julai Mwaka huu.

 

error: Content is protected !!