June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jeuri imemponza Kerry

Spread the love

UONGOZI wa klabu ya Simba kupitia Kamati Kuu ya Utendaji umemsimamisha kazi kocha mkuu wa klabu hiyo Dylan Kerry jana baada ya Klabu ya Simba kutofanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar inayotarajiwa kuisha leo visiwani Zanzibar. Anaandika Regina Mkonde … (endelea)

Klabu ya Simba ilitolewa kwenye hatua za nusu fainali baada ya kupigwa bao 1 -0 na timu ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Simba Sc imekuwa na matokeo mabaya kwenye michuano hii pamoja na michuano iliyosimamishwa kwa muda ili kupisha michuano mbalimbali iliyofanyika ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Wekundu wa msimbazi Simba, msimu huu wamekuwa na matokeo mabaya huku Simba ikiachwa nyuma na mahasimu wao walio watoa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya 3 huku Azam ikishika nafasi ya 2 na Yanga kuwa kileleni hadi sasa kwenye msimamo wa ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.

Mashabiki wa Klabu ya Simba wameupongeza uongozi wa klabu yao kwa hatua za kumsimamisha kazi kocha Kerry kwani kocha huyo alijawa na kiburi,jeuri na ukorofi,pia mashabiki hao walidai kuwa hakuwa na ujuzi wa kuchagua kikosi cha wachezaji 11 wa kwanza maarufu kama first eleven.

Mmoja kati ya shabiki wa Wekundu wa Msimbazi Simba Sc alisema kuwa kwenye mechi zilizochezwa kulikuwa na mapungufu mengi hasa ya kiufundi,kocha aliwachagua wachezaji ambao hawana viwango na kuwaacha wenye viwango.

“Kocha alikuwa hana msaada wowote kwenye timu,mechi zote tulizocheza wachezaji hawakuwa na viwango na hii yote ni sababu ya kukosa mazoezi,goli tulilofungwa na Mtibwa hatukustahili kufungwa ni uzembe wa mchezaji Peter Manyika alifanya uzembe hadi tukafungwa,mpira mzuri hauonekani uwanjani hasa kipindi cha pili.”Alisema Shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mtitu

Mashabiki hao walisema kuwa klabu yao haina desturi ya kukurupuka ya kuwafukuza makocha kama inavyotafsiriwa na baadhi ya watu kwani hadi sasa klabu imewafukuza makocha 3 ambao ni Patrick Phirry,Milovan Silcovic na Kerry,makocha wasaidizi waliamua kuondoka wenyewe kutokana na ukorofi wa Kerry kama kocha msaidizi Suleiman Matola .

“Makocha waliofukuzwa ni watatu kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wa timu,wengine waliondoka kutokana na ukorofi wa kocha mkuu.”Alisema shabiki mmoja ambaye hakulitaja jina lake

Aidha uongozi wa Simba umetakiwa kujikosoa kwa baadhi ya makosa wanayofanya ili kuijenga timu upya na si kuwahukumu wachezaji na makocha tu.

“Uamuzi wa klabu wa kumfukuza kocha mkuu nimeukubali ila kwa upande wa pili viongozi wa klabu wakaechini,watafakari makosa yao ili wajirekebishe na si kuhukumu wachezaji na makocha tu,wakati mwingine wachezaji na makocha wanakuwa hawana matatizo ila uongozi ndiyo huwa chanzo cha matatizo.”Alisema Shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Macho

Mwanahalisi Online ilijitahidi kumtafuta Msemaji mkuu wa Klabu hiyo Haji Manala kwa njia ya simu ili kupata uhakika wa taarifa hizi lakini hakupokea simu na kwa wakati huo alikuwa hajafika ofisini kwake.

Timu ya Simba ipo chini ya uongozi wa kocha msaidizi Jackson Mayanja kwa muda hadi uongozi wa klabu utakapopata kocha mpya.

error: Content is protected !!