May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jeshi la Polisi Tanzania lafumua mwongozo kazi wake

Spread the love

 

JESHI la Polisi nchini Tanzania, limezindua mwongozo wake wa utendaji kazi (PGO), baada ya kuufanyia marekebisho ili kuongeza ufanisi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano, tarehe 25 Agosti 2021, mkoani Dar es Salaam.

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), nchini Tanzania, Simon Sirro, amesema miongoni mwa marekebisho yaliyofanyika katika muongozo huo, ni urasimishaji wa madawati ya kijinsia, ili kuongeza nguvu katika mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.

“Jeshi la Polisi tumekuwa tukifanya kazi kubwa chini ya mwongozo wetu kuhakikisha tunalinda usalama wa raia na mali zao. Lakini kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini, ilitulazimu kuanzisha madawati maalumu ya jinsia na watoto ndani ya jeshi letu ili kushughulikia tatizo hili,” amesema IGP Sirro.

IGP Sirro amesema uundwaji wa madawati hayo, ni miongoni mwa jitihada za Jeshi la Polisi nchini, kuwalinda wanawake, watoto na makundi maalum dhidi ya ukatili wa kijinsia.

“Uundwaji wa madawati haya ilikuwa ni jitihada mahususi za kiu ya kutaka kuwalinda wanawake na watoto, dhidi ya ukatili mbalimbali ingawaje madawati haya hayakuwa yameingizwa rasmi katika amri ya jumla ya Jeshi la Polisi au mwongozo wa jumla wa utendaji wa jeshi,” amesema IGP Sirro.

Mbali na mwongozo huo kutambua madawati ya kijinsia, IGP Sirro amesema utatambua mtandao wa askari wanawake, kama sehemu muhimu ya jeshi hilo kuendelea kukabiliana na kesi za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto nchini.

“Ndani ya Jeshi la Polisi kuna mtandao wa askari wanawake nchi nzima, ambao nao umekuwa ukifanya kazi nzuri kila kukicha kuhakikisha haki na ustawi wa maendelo ya wanawake na watoto unalindwa,” amesema IGP Sirro na kuongeza:

“Katika maboresho yaliyofanyika ya mwongozo wetu, mtandao huo, nao umerasimishwa ili kuchochea jitihada zetu pamoja kama jeshi kuendelea kulinda usalama wa raia wote, hususani wanawake na watoto.”

Maboresho hayo yalifanyika baada ya Jeshi la Polisi nchini, kuingia makubaliano na Shirika lisilo la kiserikali, linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania, Legal Services Facility (LSF).

Ambalo lilitoa fedha kiasi cha Sh.400 milioni, kwa ajili ya kuendesha mchakato mzima wa kupitia upya mwongozo uliokuwepo awali na kuangalia maeneo ambayo yanaweza kuboreshwa zaidi ili kuendelea kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu LSF, Lulu Ng’wanakilala, amesema kukamilika kwa mapitio na maboresho ya mwongozo wa jeshi hilo, ni sehemu ya mkakati wa shirika lake kwa kushirikiana na Serikali, katika kufanya uchechemuzi.

Pamoja na kuleta mabadiliko ya sera, sheria na miongozo ya uboreshwaji ustawi wa haki na maendeleo ya wanawake nchini.

“Uzinduzi huu una maana kubwa sana kwetu, kama shirika binafsi linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania. Hii ni sehemu ya ushirikiano wetu na Jeshi la Polisi kupitia makubaliano tuliyotiliana saini, ili kuweza kusaidia zoezi la kuupitia upya mwongozo wao,”

“Ili kurasimisha kabisa madawati ya jinsia, ambayo yamekuwa yakifanya kazi kubwa ya kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto nchini Tanzania,” amesema Ng’wanakilala.

Ng’wanakilala amesema mwongozo huo ulioboreshwa, utasaidia watu wote hasa wanawake na watoto, ambao ni kundi linalohitaji zaidi msaada wa kisheria kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo nyumbani na katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

error: Content is protected !!