October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Jeshi la Polisi laonya watoa taarifa za uongo kuhusu Corona

Spread the love

JESHI la Polisi nchini limeonya watu wanaosambaza taarifa zisizo sahihi, kuhusu mlipuko wa Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu inayosababaishwa na Virusi vya Corona (COVID-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Onyo hilo limetolewa leo tarehe 21 Machi 2020 na SACP David Misime, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, wakati akitoa ujumbe wa jeshi hilo kwa wananchi kuhusu udhibiti wa mlipuko huo.

SACP Misime amewataka Watanzania kuepuka kusambaza taarifa za uongo juu ya ugonjwa huo, huku akiwasisitiza kufuatilia taarifa zinazotolewa na viongozi wa serikali au mamlaka za afya.

“Tuendelee kufuata maelekezo tunayopewa na viongozi wa kitaifa na watalaamu wa afya, epuka kusambaza taarifa za kuzusha zisizo sahihi na zinazotakia wengine mabaya,” amesema SACP Misime.

Wakati huo huo, SACP Misime amewataka wananchi kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria, vitakavyopelekea kukamatwa na kuwekwa mahabusu ambako kuna mkusanyiko wa watu wengi, na kuhatarisha maisha yao.

 “Ujumbe wa polisi katika kipindi hiki cha kuzuia na kudhibiti virusi vya Corona, tuthamini afya zetu na za wanzetu kwa kutii sheria. Epuka kutenda kosa la uhalifu iwe dogo au kubwa kwani itakusababishia kukamatwa na kuwekwa mahabusu na kukuingiza katika mikusanyiko itakayoweza kukusabaisha kuambukizwa Corona,” ameshauri SACP Misime.

error: Content is protected !!