VIONGOZI wa mapinduzi ya kijeshi nchini Niger wametangaza kuwa na ushahidi wa kumshtaki rais aliyeondolewa madarakani na washirika wake wa ndani na nje kwa uhaini mkubwa pia kwa kuhatarisha usalama wa ndani na nje wa Niger. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa …(endelea).
Rais wa Niger, Mohamed Bazoum ambaye aliondolewa madarakani na kuzuiliwa tangu tarehe 26 Julai 2023 baada ya mapinduzi yaliyoongozwa na wanajeshi, anakabiliwa na shutuma mpya kutoka kwa jeshi hilo.
Jeshi ambalo liliunda serikali katika kipindi hiki cha machafuko nchini Niger, jana Jumapili limetangaza kwamba wana nia ya kumshtaki mkuu huyo wa nchi aliyeondolewa mamlakani kwa uhaini na kwa kuhatarisha usalama wa nchi.
Kanali Meja Amadou Abdramane ambaye ni mmoja wa wajumbe wa serikali, katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa imebainisha kuwa rais huyo anayezuiliwa alirekodiwa njia ya simu.
Mohamed Bazoum, familia yake na washirika wake kadhaa wa karibu bado wanazuiliwa katika chumba cha chini cha makazi ya rais huko Niamey.
Siku ya Jumamosi tarehe 12 Agosti 2023, rais wa Niger alitembelewa na daktari wake wa kibinafsi.
Kulingana na daktari huyo, wote wanaozuiliwa wanaendelea vyema na Mohamed Bazoum naye iko vizuri kiafya.
Hata hivyo, Rais Bazoum alisema kuwa matibabu yaliyotengwa kwa ajili ya familia yake na yeye mwenyewe ni ya kinyama na ya kikatili.
Jana Jumapili, mamlaka ya kijeshi pia ilishutumu vikwazo haramu, vya kinyama na vya kufedhehesha vilivyowekwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo inapinga mapinduzi hayo na kutishia kuivamia nchi hiyo ili kurejesha utawala wa kikatiba, ingawa njia ya diplomasia inapendekezwa kila wakati.
Leave a comment